Mahakama Yamwachia Kulthum Mansoor Wa TAKUKURU

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia kwa dhamana aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kulthum Mansoor (57) aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi baada ya kufutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha na kubaki mashtaka saba.

 

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwasilisha ombi la kubadilisha hati ya mashtaka baada ya kumfutia mshtakiwa huyo mashtaka ya utakatishaji fedha na hivyo kupewa dhamana.

 

Akisomewa masharti ya dhamana mshitakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini wawili  wenye barua na vitambulisho vya Taifa au vitambulisho vinavyotambulika watakaosaini  bondi ya Sh. milioni 20.

Mansoor ametimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili.

 

Wakili wa Serikali Sylvia Mitanto amedai kuwa miongoni mwa mashtaka hayo mapya ni shtaka analodaiwa kuwa kati ya Januari  2013 na Mei mwaka 2018 akiwa mtumishi wa Takukuru alighushi barua ya Agosti 13,2003 kwa lengo la kuonesha  imetolewa na Halmashauri ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Agosti 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.


Toa comment