The House of Favourite Newspapers

MAHAKAMA YAMWACHIA BWEGE, POLISI WAMSWEKA RUMANDE

MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara maarufu kwa jina la Bwege na viongozi waandamizi wa hicho, huku Jeshi la Polisi likiendelea kuwashikilia kwa kilichotajwa kuwa wamekosea usajili wa majina yao.

 

Bwege na wenzake ambao ni Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Mbarala Maharagande, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa, Abuu Mjaka na mjumbe wa Kamati Tendaji, walikamatwa na polisi juzi Jumanne, kwenye kampeni za udiwani Kata ya Kivinje, Kilwa.

 

Kwenye mahakama hiyo, watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka matano yakiwamo ya uchochezi.

 

Katika Shitaka la kwanza ambalo ni la uchochezi, watuhumiwa wote watatu wanashtakiwa kwa tuhuma za kutamka maneno yanayoweza kuhatarisha amani kwenye mkutano wa kampeni za udiwani kwenye Kata ya Kivinje.

 

Shtaka la pili ni linamkabili Mbunge Bungara ambaye anatuhumiwa kutamka maneno ya kutishia amani huku shtaka la tatu likishindwa kusomwa kutokana na mtuhumiwa wa kosa hilo ambaye ni Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali kutokuwepo mahakamani hapo.

 

Shtaka la nne linamkabili Maharagande, ambaye anatuhumiwa kutamka maneno ya vitisho kwenye hadhara na shtaka la tano linamkabili Mjaka kutuhumiwa kutoa maneno ya matusi kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo anadaiwa kusema “ukimuona mwana CCM ujue huo mshipa wake wa akili umeungana na mshipa wa mavi.”

 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 3, mwaka huu huku watuhimiwa wakiachiwa kwa dhamana ya mahakama yenye masharti ya kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja na dhamana ya maandishi ya Tsh. Milioni 1.

 

Baada ya kukamilishwa kwa taratibu hizo jeshi la polisi liliendelea kuwashikilia viongozi hao kwa kilichodaiwa kuwa wamekosea kuyasajili majina yao hivyo polisi ikasema muda umekwisha, na watuhumiwa kuendelea kushikiliwa hadi kesho asubuhi.

AJIUA KIKATILI KISA PENZI LA BINAMU YAKE – VIDEO

Comments are closed.