The House of Favourite Newspapers

MAHAMANI kwa Kuandika “Kawatembelea Ukerewe Siku 2 Tu, Wakafa”

MKAZI wa Mwanza, Emmanuel Mahumbi (38) jana amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

 

Inadaiwa Septemba 2018 katika Jiji la Dodoma, Mahumbi alichapisha taarifa za uongo katika mtandao wa facebook zikisema; “Kichaa m1 anatoa kafara kiboya kweli kaenda kumuona dada yake Bugando kumbe ndio anaenda kumkabidhi Freemason cku moja 2 baada ya kukuona akafa na kufa 2/ kaenda kuwatembelea Ukerewe cku 2 tu baada ya kuwaona wakafa na kufa kumbe alienda kuwakabidhi kwa freemason boya kweli liambieni libadilike litamaliza watu”.

Mahumbi alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Mmbando.

 

Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo katika tarehe isiyofahamika Septemba mwaka jana jijini Dar es Salaam. Mshitakiwa alikana mashitaka, na upande wa mashitaka umedai kwamba, upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo wameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu ameiomba Mahakama hiyo impatie dhamana mshitakiwa kwa sababu makosa yake yana dhamana na kwamba impe masharti nafuu kulingana na mashitaka yake. Wakili Martin alisema, hawana pingamizi na dhamana, lakini watoe masharti ambayo yatamlazimu mshitakiwa kuwepo mahakamani wakati anapohitajika.

 

Hakimu Mmbando alimtaka kuwa na wadhamini wawili wanaotoka ofisi zinazotambulika ambao watasaini bondi ya Sh milioni 10 na kuwasilisha hati ya kusafiria. Mshitakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi imeahirishwa Februari 28, mwaka huu.

 

Comments are closed.