The House of Favourite Newspapers

Maisha rahisirahisi

0

MFUMO wa mafanikio umejengwa kwenye mambo magumu.  Huhitaji kupiga ramli kujua kama utafanikiwa au la.  Kipimo chako ni jinsi unavyojiepusha na masuala rahisirahisi.

Utajiri siyo rafiki wa mtu mwenye kuchagua vitu vyepesi. Kama nilivyosema hapo juu ni rahisi sana kujua kama wewe utakuwa masikini milele kwa kujiangalia namna unavyofanya mambo yako.

Kama ni mfanyakazi ambaye furaha yako iko kwenye kutegea kazi, ukulima wako ni wa kizembe, kusoma kwako ni izeize, biashara yako unaiendesha kizembezembe tambua kuwa nafasi uliyochagua ni ya umaskini wa milele wala usitegemee uchawi.

Pamoja na kwamba urahisi ni mbegu ya umaskini kuna madhara mengine ambayo yanaweza kumpata mtu anayependa kuishi katika mfumo wa kirahisi rahisi ambayo ni haya yafuatayo:

MSONGO WA MAWAZO

Mtu mzembe ni rafiki wa msongo wa mawazo kwa sababu upatikanaji wa mahitaji ya kimaisha ni mgumu. Ni wazi mtu wa maisha rahisirahisi kila siku atajikuta hapati anachohitaji hivyo kumsababisha awe mwenye mawazo na kuwaonea gere wenzake wanaofanikiwa.

Kibaya zaidi ni kwamba msongo wa mawazo ndiyo mashine inayofua madhara makubwa sana ya kiafya hivyo kumweka mtu katika hatari ya kufa mapema au kukumbwa na magonjwa ya mara kwa mara.

MUUMINI WA BAHATI MBAYA

Msomaji wangu, kama umewahi kuwasikia watu ambao ni wafuasi wa bahati mbaya, msingi wao mkubwa ni uzembe na kuishi maisha mepesi.

“Nilikuwa natembea barabarani bahati mbaya nikagongwa na gari, bahati mbaya nimepoteza fedha, bahati mbaya nimefukuzwa kazi.”

Hizi ni kauli za watu wanaoishi maisha rahisi.

Maana sote tunajua uzembe ndiyo mwanzo wa bahati mbaya, hili halina ubishi ingawa hata umakini wakati mwingine hauondoi matukio ya bahati mbaya, lakini ni kwa kiasi kidogo sana,  tofauti na mtu mzembe.

KUTOAMINIKA

Kuaminika ni jambo muhimu sana katika maisha, mtu ambaye haaminiki katika jamii anakuwa sawa na binadamu anayeishi katika dunia yake. Ni vigumu kuchanganyika na wenzake na kuwa na maisha ya furaha.

“Aaa…nani?  Fulani huyo usimwajiri, msimpe nafasi, msimwachie kazi peke yake ataharibu, hawezi.” Maneno hayo hutokea katika maisha ya mtu wa kutengwatengwa, huwa ni sehemu ya maisha ya watu wanaoishi kirahisi rahisi. Zaidi ya hapo mzembe huwa hajiamini hata mwenyewe, jambo linalomuondolea ujasiri wa kuishi na wenzake.

UELEWA MDOGO

Maisha rahisi hayaongezi ufahamu. Sayansi ya akili inabainisha kuwa namna pekee ya kukua kiakili ni kutafuta majibu ya vitu vigumu. Binadamu asiyekumbana na changamoto kwenye maisha yake hawezi kuendelea.

Uchunguzi unaonyesha kuwa hata wagunduzi wa ndege, simenti, magari na vitu vingine vya kitaalamu walifanikiwa katika ugunduzi wao wakati wakikabiliana na maisha magumu, wakitafuta majibu ya changamoto zao.

Nashauri tuishi kwa kukabili changamoto siyo kuzikwepa kwa kutafuta maisha mepesi.  Asante kwa kunisoma!

Leave A Reply