The House of Favourite Newspapers

MAISHA YA GEREZANI YA VIGOGO KESI ZA TRILION 2.5 UKWELI WAANIKWA

 

YAPO madai mengi mtaani kuhusiana na wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa wanaopelekwa mahabusu ama kwa kunyimwa dhamana au kufungwa.  Kwamba, kuna upendeleo unaofanywa wakiwa huko juu ya maisha yao, sasa ukweli wa madai hayo umeanikwa. Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi walidai kwamba wafanyabiashara na maofisa mbalimbali wa idara za Serikali au kampuni binafsi ambao wapo mahabusu kwenye magereza mbalimbali kutokana na madai ya kuitia hasara Serikali au kupoteza zaidi ya shilingi trilioni 2.5, wanaishi kwa raha ‘kama malaika’.

 

Wapo waliodai na wanaoamini kuwa huwa vigogo hao hawapati shurba wanazozipata watu wa kawaida wasio na nyadhifa. Akizungumza na Gazeti la Uwazi katika mahojiano maalum, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, SP Amina Kavirondo (pichani) alichambua madai hayo huku akitoa mifano.

 

KUTENGWA KWENYE KULALA

Baadhi ya wananchi hao walidai kuwa, kuna baadhi ya wenye fedha huhonga ili waishi maisha mazuri gerezani kisha kulala sehemu maalum na wengine hutoroshwa usiku kwenda kuona ndugu zao, Kamanda Kavirondo alisema wanaosema hivyo hawajui sheria za magereza.

 

“Nikujibu kwa uhalisia, gereza halina class (madaraja), gereza halina vyumba na kama tungekuwa na vitu hivyo tungelalamika nafasi, labda kama ni mgonjwa au anahitaji uangalizi fulani. “Yeyote yule akiingia gerezani ataishi kama mahabusu au wafungwa wengine, hatuna first class au second class. Wapo waliopitia humu mnawajua, mnaweza kuwauliza.

 

KUTOROSHWA NJE YA GEREZA USIKU

Akijibu kuhusu madai ya mfungwa au mahabusu kuwa na uwezekano wa kuroshwa usiku, Kamanda Kavirondo alisema hilo ni jambo lisilowezekana kabisa. “Mahabusu au mfungwa anapoingia gerezani hukabidhiwa kwa makabidhiano maalum na hata anapokwenda nje ya gereza, mkuu wa gereza, mkuu wa magereza mkoa na mkuu wa magereza nchini lazima wanawajua wanaotoka.

 

“Gereza likishafungwa hakuna mtu wa kufungua labda kwa amri ya mkuu wa magereza na taarifa kupelekwa makao makuu. “Mtu anayejua sheria za magereza hawezi kusema hivyo kwani wakati wa kuingizwa selo huhesabiwa na viongozi akiwepo mkuu wa magereza na rekodi zinatumwa hadi makao makuu ya jeshi.”

 

CHAKULA WANACHOKULA

Alipoulizwa kuhusu chakula, kwamba kuna madai kuwa wengine hawali chakula cha magereza, kamanda huyo alisema mahabusu yeyote yule ni mtuhumiwa na ndiyo maana huwa hawavai sare za wafungwa kwa kuwa mahakama haijathibitisha makosa yake hivyo anaweza kula chakula cha nje kutoka kwa familia yake.

 

“Hicho chakula lazima kiombewe kibali na atapewa taratibu za kuingiza chakula, kwa kujaza fomu maalum na lazima iwepo na picha yake. Lakini mfungwa anahudumiwa chakula na Serikali,” alisema Kamanda Kavirondo.

 

SIMU ZA MKONONI

Alipoulizwa kuhusu wafungwa au mahabusu kutumia simu wakiwa magereza na kuwasiliana na watu wa nje kama kawaida, alisema Jeshi la Magereza haliruhusu mahabusu au mfungwa kuingia na simu gerezani.

 

“Akiwa na shida na familia yake, zipo taratibu za kuwasiliana na ndugu zake kwa mujibu wa sheria na huwa hawapewi simu kabisa. Zipo njia mbalimbali za wafungwa au mahabusu kuwasiliana na ndugu zao na zinaratibiwa na viongozi wa gereza,” alisema.

 

BAADHI YA VIGOGO WALIO MAGEREZANI

Baadhi ya viongozi walio mahabusu katika magereza jijini Dar es Salaam ni pamoja na wale vigogo sita wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa zamani, Dickson Maimu ambao tayari wamefikishwa mahakamani na kusomewa hati mpya ya mashtaka 100 yakiwamo 22 ya kughushi, nyaraka za kumdanganya mwajiri 43, kujipatia fedha, matumizi mabaya (moja) na kutakatisha fedha na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya shilingi bilioni 1.175.

 

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Aveline Mombuli, Astery Ndege, George Ntaliwa, Xavery Silverius maarufu kama Sliverius Kayombo na Sabina Nyoni. Walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Salum Ally. Upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Leonard Swai. Wankyo alidai kuwa kesi hiyo namba 07/2019 ina mashtaka 100 dhidi ya washtakiwa hao.

 

KITILYA NA WENZAKE

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Harry Kitilya na wenzake, Shose Sinare ambaye alikuwa Ofisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic na Sioi Solomon ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Benki ya Stanbic, nao ni miongoni mwa vigogo ambao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka nane.

 

Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa katika mahakama hiyo ni pamoja na kutakatisha fedha, kujipatia fedha kinyume cha sheria, kughushi nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda kati ya Agosti 2012 na Machi 2013.

 

Watuhumiwa hao walidaiwa kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya kughushi dola milioni 6, kama malipo ya kufanikisha Serikali ya Tanzania kupata mkopo wa dola milioni 550 kutoka Benki ya Stanbic ya jijini London, Uingereza, mkopo ambao ulipitia Benki ya Stanbic Tawi la Tanzania. Watuhumiwa hao wote walikana makosa na wapo rumande.

 

RUGEMALIRA NA SETH

Wafanyabiashara James Rugemalira na Harbinder Singh Sethi ‘Singasinga’, wanadaiwa kujipatia kwa ulaghai kutoka Benki Kuu (BoT) dola 22,198,544.60 za Kimarekani na shilingi 309,461,158.27 za Kitanzania kati ya Novemba 28, 29, 2011 na Januari 23, 2014 wakiwa Makao Makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Kinondoni na Benki ya Mkombozi, Tawi la St Joseph jijini Dar.

 

Kiasi hicho cha fedha kimewafanya wawili hao washtakiwe kwa kosa lingine la kuisababishia Serikali hasara kwa tukio lililotokea Novemba 29, 2013 katika Tawi la Kati la Benki ya Stanbic.

 

DK TENGA NA WENZAKE

Wakili Dk Ringo Tenga na washtakiwa wengine ambao ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Six Telecoms, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms, wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 jijini Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Kimarekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

 

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Kimarekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato. Washtakiwa hao, wanadaiwa kwa kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Kimarekani 466,010.07 kwa TCRA.

 

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia au walisimamia Dola za Kimarekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao zililotokana na makosa ya udanganyifu wa mashitaka yaliyotangulia. Vilevile, washitakiwa hao wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Kimarekani 3,748,751.22 (zaidi ya shilingi bilioni 8 za Kitanzania).

 

MPEMBA WA MAGUFULI

Yusuf Ally maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli’ na washtakiwa wengine ambao ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya shilingi milioni 785.6.

 

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2015, wakiwa jijini Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 180,000 sawa na shilingi milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

 

MALKIA WA TEMBO

Raia wa China, Yang Feng Glan maarufu kama ‘Malkia wa Meno ya Tembo’ na wenzake wanadaiwa kati ya Januari, Mosi na Mei 22, 2014 walifanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889, vikiwa na thamani ya shilingi bilioni 5.4 bila kuwa na leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

 

RAIS ACACIA

Naye aliyekuwa Rais wa Kampuni ya Acacia, Deogratias Mwanyika na washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Alex Lugendo, Mkurugenzi Mtendaji wa Pangea, North Mara na Bulyanhulu, Assa Mwaipopo, Kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 112.

 

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2007 katika sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, Kahama mkoani Shinyanga, Tarime mkoani Mara, Biharamulo mkoani Kagera, maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa Kamishna Jenerali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kodi ya Dola za Kimarekani milioni 9.3 ambayo ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

 

Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kuwa kati ya Desemba, 2009 na Desemba 31, 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia Mgodi wa North Mara kuhamisha fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 374,243,943.45 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

 

WENGINE

Washitakiwa wengine ambao wapo magerezani kwa tuhuma mbalimbali ni pamoja na aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na katibu wake, Selestine Mwesiga na mhazini wao, Nsiande Mwanga wanaodaiwa kutakatisha Dola za Kimarekani 173,335. Wengine ni aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange almaarufu Kaburu wanatuhumiwa kutakatisha Dola za Kimarekani 300,000.

Stori: ELVAN STAMBULI NA MEMORISE RICHARD

 

 

Comments are closed.