Maisha ya Queen Darleen Kufuru

 


BAADA ya kuolewa mke wa pili na jamaa anayetajwa kuwa tajiri maarufu jijini Dar aitwaye Isihaka Mtoro, maisha ya msanii wa Bongo Fleva, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ ni kufuru tupu, Risasi Jumamosi limedokezwa.

 

Queen Darleen ambaye ni first lady wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya kaka yake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, alifunga ndoa hiyo ya kimyakimya Jumapili iliyopita jijini Dar na kushuhudiwa na watu wachache.

 

Hata wasanii wenzake wa WCB, wengi hawakuhudhuria zaidi ya kumtakia kila la heri mitandaoni.

Chanzo kimeliambia gazeti hili kuwa, mara baada ya ndoa hiyo, sasa maisha ya Queen Darleen yamebadilika kabisa.

 

Chanzo hicho kilieleza kuwa, Queen Darleen kwa sasa anajiachia kwenye mjengo wa ghorofa aliopewa na mumewe huyo uliopo Mbezi-Beach jijini Dar, jirani na nyumbani kwa Diamond au Mondi.

 

“Unaambiwa baada ya kuolewa, Queen amepewa maisha na mumewe. Sasa hivi Queen ni malkia wa ukweli maana maisha yake ya Mbezi-Beach siyo yale tuliyozoea kuyaona Sinza (Dar).

“Unaambiwa mbali na kuishi kwenye hekalu, lakini pia anabadilisha tu magari kama anavyotaka. Leo anatoka na gari hili, kesho anatoka na lingine.”

 

Baada ya kunyetishiwa ishu hiyo, Gazeti la Risasi lilizama mzigoni na kumuibukia Queen Darleen ambapo lilikaribishwa nyumbani hapo na mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Pizzy ambaye ni shemeji wa Queen Darleen.

Risasi Jumamosi: Mambo kaka! Samahani, hapa ni nyumbani kwa Queen Darleen?

Pizzy: Ndiyo ni hapa, unasemaje?

Risasi Jumamosi: Mimi ni mwandishi wa habari kutoka Global, nina shida naye…

Pizzy: Subiri hapo getini, ngoja nikamwambie Queen, akiniruhusu ndipo utaingia.

Baada ya dakika tano, Pizzy alirejea.

 

Pizzy: Yupo ghorofani anaswali, amesema ingia umsubiri.

Mwandishi wetu alizama ndani ya fensi ambapo alilishuhudia jumba la kifahari la ghorofa moja analoishi Queen Darleen.

 

Pia alishuhudia magari mawili yaliyoegeshwa nje huku ikionekana ujenzi wa eneo hilo ukiendelea na kuremba ndani ya fensi ya mjengo huo.

Baada ya kufika ndani, mwandishi wetu alikaribishwa eneo la barazani ambapo kuna makochi ya ngozi ya bei mbaya ambapo alipata fursa ya kuchungulia ndani.

 

Ndani ya nyumba hiyo alishuhudia samani za bei mbaya na urembo uliokwenda shule.

Risasi Jumamosi: Samahani kaka, kwani hapa Queen amepangisha yeye mwenyewe?

Pizzy: Hapana, nyumba hii amepangiwa na mumewe.

Risasi Jumamosi: Inasemekana ameolewa mke wa pili. Je, huyo mke wa kwanza naye anaishi hapa?

Pizzy: Hapana, kila mtu ana kwake.

 

Hata hivyo, baada ya kuswali, Queen Darleen alifuatwa ghorofani alikokuwa akijiachia kwa raha akifaidi matunda ya ndoa, lakini aliomba kama ni mahojiano ayafanye siku ya Alhamisi (juzi) kwani kutakuwa na Maulidi kwa ajili ya kusherehekea ndoa yake.

 

RISASI LATINGA

Siku ya Maulidi, Risasi Jumamosi lilitinga nyumbani hapo na kushuhudia bonge la sherehe.

Awali, alianza kuingia Nasibu Abdul ‘Diamond’ na mpenzi wake Tanasha Donna huku wakiwa wameshikana mikono jambo lililozua gumzo kwa watu kwani wengi wao walifikiri Tanasha ametimka mazima Bongo.

 

Baada ya Diamond na mzazi mwenziye huyo, mshereheshaji aliwaruhusu bwana na bibi harusi waingie, ndipo Queen Darleen na mumewe wakaingia na kuibua shangwe kwa wageni waalikwa.

 

SHEHE AZUNGUMZA

Shehe aliyemuozesha Queen, Muharami Mziwanda naye alipewa kipaza sauti ambapo aliwasihi wanandoa hao waishi vizuri kwa upendo, furaha na amani.

Kama hiyo haitoshi, alimfagilia mume wa Queen Darleen kuwa siyo mtu wa njaa njaa.

 

“Kwa ambao hamumjui huyu Isihaka hana njaa njaa hata kidogo, yupo vizuri kweli. Mimi mwenyewe kanijengea nyumba kubwa tu tena siyo nyumba ni bonge la mjengo wa thamani kaniweka pale shehe wake nafurahia maisha kwa hiyo msije mkasema ooh kaamua kumuoa Queen Darleen kwa sababu ya umaarufu wa kaka yake Nasibu, hapana,” alisema Shehe Muharami huku akishangiliwa na wageni waalikwa ukumbini hapo.

 

Baada ya shehe kumaliza, lilifuata tukio la pete ambapo Isihaka alimvisha pete mkewe Queen na kisha kukata keki na kulishana.

Baadaye ndipo muda wa chakula ukawadia, watu wakala na kunywa kisha ikafuata burudani ya kibao kata ambapo watu walicheza na kufurahi.

 

Mwanamama machachari kwenye muziki wa Taarabu, Khadija Kopa naye alitumbuiza pamoja na wasanii wengine.

Sherehe hiyo ilipata baraka pia kwa kuhudhuriwa na baba Diamond, Abdul Juma na baba wa kufikia wa msanii huyo, Maisara Abdul ‘Shamte’ ambao walikaa pamoja.

 

Mbali na Diamond, wasanii wengine waliokuwepo kwenye shughuli hiyo ni pamoja na Lavalava, Khadija Kopa, Dula Makabila, Gigy Money na meneja wa wasanii Petit Man.

STORI: MEMORISE RICHARD NA IRENE MARANGO

Toa comment