The House of Favourite Newspapers

Maisha ya wasiwasi na jinsi ya kukabiliana nayo

0

????????????????????????????????????

UKICHUNGUZA kwa makini utabaini kuwa watu wanaoishi katika hali ya umaskini ndiyo wanaoongoza katika maisha ya wasiwasi, tofauti na wale waliofanikiwa kimaisha.

Kwa maskini, fikra za kuuguza ni nzito maradufu kwa sababu huambatana na maswali: “Nitafanyaje mwanangu akiugua na mimi sina fedha za matibabu?”

Kwa msingi huo, maisha ya wasiwasi ni kipimo kikuu cha udhaifu wa mtu katika kushughulikia changamoto zinazomkabili kwenye maisha yake ya kila siku.

Ni rahisi mtu kujua anawajibika kwa kiwango gani katika kukabiliana na matatizo kwenye maisha yake kwa kujitathmini ni mwoga wa maisha kwa asilimia ngapi?

Ukimsikia mtu anasema naogopa hili na lile likinikuta ujue amekosa au hajajenga nyenzo za kulivuka tatizo husika. Kisaikolojia si rahisi mwanadamu kuhofu kitu ambacho anaweza kukabiliana nacho na kukishinda.

Wamasai hawamuogopi mnyama simba si kwa sababu ni mpole bali pamoja na ukali wake wanajiamini katika kumkabili na kumshinda, hivyo ndivyo ilivyo katika matatizo yanayotukuta kila siku kwenye maisha yetu.

Katika hali ya kawaida hakuna wasiwasi unaoshinda ujumla wa wanadamu wote isipokuwa kifo.  Nacho ni kwa sababu moja tu kwamba hajatokea mwenye kukabiliana nacho na kukishinda, lakini mambo mengine yanatofautiana kati ya mtu na mtu.

Wapo wanaoogopa kufungwa jela lakini kuna wengine wanatamani waishi huko milele na milele. Kama hilo ni nusu fikra, yapo mengi ya kujilinganisha, kwa mfano, wasiwasi wa kuugua hauwatishi watu wote kwa sababu kuna wanaojiamini kuwa wana uwezo wa kwenda nchi mbalimbali za Ulaya na kujitibu kwa gharama yoyote  wakapona.

Miaka michache iliyopita nilikuwa na wasiwasi wa kuishi maisha ya peke yangu.  Nilijiuliza nitakula nini?  Nitapata wapi fedha za kulipa kodi ya chumba?  Nitawezaje kufanya hili na lile kwenye maisha yangu binafsi?

Bila shaka mawazo hayo yalitokana na uwajibikaji wangu mdogo katika kupata majibu niliyokuwa najiuliza.

Baada ya kujituma katika kutafuta majibu ya changamoto zilizokuwa zinanikabili, hofu ya maisha ya kupanga haipo tena, najiona niko salama hata kama nikimkuta mwenye nyumba amenuna  naamini nitaweza kutafuta mahali nikaishi na familia yangu.

Karne hii ni ya kila mtu kuachana na maisha ya wasiwasi ambayo ni hatari sana katika afya zetu.  Mwanzo wa kuishinda hofu ni kupambana na kile tusichokuwa nacho ambacho kwa namna moja ama nyingine ndicho kinachotutia hofu.

Msomaji wangu, chukua muda ujiulize una wasiwasi juu ya nini kwenye maisha yako? Kile unachokiogopa tambua kuwa hujakitafutia nguvu ya kukishinda. Njia pekee ya kuondoa hofu ni kutafuta kinga thabiti itakayokufanya ujiamini kuwa  tayari kwa mapambano.

Yawezekana unaogopa uchawi; lakini njia za kushinda uchawi si zipo?  Kwa nini usizifuate?   Jenga imani yako kwa kufuata misingi ya dini au jiamini mwenyewe kuwa huwezi kudhurika kwa uchawi.  Ukifanya hivyo kikwazo cha wasiwasi huo utakivuka na utaishi kwa amani.

Ninapofundisha somo hili kuna baadhi wanaweza kujiuliza kwamba mtu maskini anawezaje kuishi mbali na wasiwasi ilhali hana kitu? Ukosefu wa kitu ndiyo chanzo cha tatizo, tafuta njia ya kufanya ili upate mafanikio yatakayokukinga na wasiwasi usiokuwa na sababu.

Akiba ya 100,000 ni kubwa kwa mtu ambaye maisha yake ni ya kawaida kwa sababu atakuwa ameweka wazi jibu la nitafanyaje mtoto akiugua usiku? Kwake yeye jibu litakuwa nitakwenda benki na kuchukua 50,000 kisha nitampeleka mwanangu zahanati.

Bila shaka jibu hili ni la matumaini, tofauti na mtu ambaye hana kitu kabisa.

Leave A Reply