The House of Favourite Newspapers

Maisha Yanakwenda Kasi Sana Man U

0

M A N CH ESTER, England

 

CRISTIANO Ronaldo amerejea Old Trafford baada ya miaka 12 kupita, mchezo wake wa mwisho kama mchezaji wa timu hiyo kipindi hicho ilikuwa ni dhidi ya Barcelona kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mei 27, 2009, Man United ikipoteza kwa mabao 2-0.

 

Wikiendi iliyopita katika mchezo wake wa kwanza kikosini hapo, alifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Newcastle United pale Old Trafford ukiwa ni mchezo wa Premier.

 

Juzi Jumanne, alicheza mechi yake ya pili dhidi ya Young Boys katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, alifunga bao moja wakati wakipoteza kwa mabao 2-1 ugenini.

 

Kuna vitu ambavyo vimetokea tangu Ronaldo aondoke Man United mwaka 2009 mpaka anarejea.

 

MAISHA YAKE UNITED

Kurejea kwa Ronaldo kikosini hapo, zilikuwa zimepita takribani siku 4488. Wakati anaichezea Man United, alitwaa mataji matatu ya Premier League, mawili ya FA na Carabao Cup, pia Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Klabu Bingwa Dunia, Tuzo ya Ufungaji Bora na Ballon d’Or.

 

Alifunga mabao 118 na kutoa asisti 69 katika mechi 292.

 

Katika msimu wake wa mwisho ndani ya Man United, alishinda taji la Premier, huku akitawala dabi zote dhidi ya Manchester City.

 

Baada ya kuondoka kwa staa huyo, Man City walianza kufanya uwekezaji kwa kusajili wachezaji wa daraja la juu kama Carlos Tevez, Sergio Aguero, David Silva na Kevin De Bruyne ambapo walitwaa mataji matano ya Premier, FA (2), Carabao Cup (6) na Ngao ya Jamii (3).

 

Bila Ronaldo, Man United walitwaa mataji mawili ya Premier, FA (1), Carabao Cup, Ngao ya Jamii (3) na Europa League (1).

 

Man United waliko sekana kwenye Ligi ya Mabingwa mara tatu, tangu mwaka 2017 hawajashinda taji lolote mpaka sasa.

 

Man United walitawala soka la Premier kwa miaka 12 iliyopita, lakini Chelsea, Liverpool na Arsenal walibaki kuwa wapinzani wakubwa wa timu hiyo.

 

Baada ya Ronaldo kwenda Madrid mwaka 2009, Arsenal walishi ndwa kutamba na nafasi yao ikachukuliwa na Tottenham ambao walipenya ndani ya big six, huku Leicester City wakitwaa taji la Premier msimu wa 2015/16.

 

UZITO WA JEZI NAMBA 7

Tangu alipoondoka Ronaldo, wachezaji kadhaa ndani ya Man United walikabidhiwa jezi namba saba akiwemo Michael Owen (2009-12), Antonio Valencia (2012-14), Angel Di Maria (2014-15), Memphis Depay (2015-17) na Alexis Sanchez (2017- 19), kati ya hao, hakuna ambaye aliweza kuitendea haki.

 

Msimu uliopita Edinson Cavani alivaa jezi hiyo, akafunga mabao 17 katika mechi 39. Msimu huu Ronaldo amerejea na kukabidhiwa jezi yake, kilichobaki ni kuendeleza pale alipoishia.

 

MAPAMBANO BILA FERGUSON

Kocha Sir Ferguson aliibadili Man United kuwa timu yenye mafanikio ndani ya Premier, aliondoka mwaka 2013 baada ya kustaafu kufundisha.

 

Tangu alipoondoka, United haijashinda tena taji la Premier na Ligi ya Mabingwa Ulaya, mara ya mwisho kufika mbali kwenye michuano hiyo ilikuwa mwaka 2011 ilipocheza fainali.

 

Timu hiyo imetumia euro bilioni 1.35 kwenye usajili kipindi cha makocha David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho.

 

REKODI ZAKE

Ronaldo ambaye aliondoka kikosini hapo akiwa na miaka 24 kipindi kile sio wa sasa ambaye amerejea akiwa na miaka 36.

 

Akiwa Madrid, Ronaldo alifunga mabao 451 katika mechi 438 na kuwa mfungaji bora wa muda wote katika klabu hiyo akiwa na wastani wa 1.03 wa kufunga kwa mechi.

 

Katika msimu ambao alikuwa vibaya alifunga mabao 33 ndani ya Madrid, lakini msimu wa 2011/12 alifunga mabao 60 na 2014/15 alifunga mabao 61.

 

Aliipa Madrid mataji 15, yakiwemo manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu tisa kabla ya kwenda Juventus ambako alifunga mabao 101 katika mechi 138.

 

Ameshindaji taji la Euro 2016, amefunga mabao 786 akiwa na kikosi cha Ureno. Ndani ya timu ya taifa, ana mabao 111. Ndiye mchezaji wa kiume mwenye mabao mengi zaidi kwenye rekodi za timu za taifa.

 

Pia ndiye mfungaji bora wa muda wote na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na mabao 136, pia ni mfungaji wa muda wote ndani ya Euro akiwa na mabao 14.

Leave A Reply