The House of Favourite Newspapers

Wanasayansi Wagundua Maiti ya Kale ya Mjamzito Misri

0

TIMU ya wanasayansi nchini Poland imesema wamegundua maiti pekee ya kale ya mwanamke mjamzito huko Misri iliyokuwa imehifadhiwa.

 

Ugunduzi huo umebainika na wanasayansi wa eneo la hifadhi ya maiti la Warsaw na kuandikwa katika jarida la Sayansi la Akiolojia.

 

Hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015, na inatumia teknolojia ya kisasa kutathmini viti vya kale vilivyohifadhiwa katika Makubusho ya Taifa iliyopo Warsaw.

 

Awali, maiti hiyo ilikuwa ikidhaniwa kuwa ya kasisi wa kiume lakini uchunguzi wa CT Scan ukaonesha kuwa ni maiti ya mwanamke aliyekuwa hatua ya mwisho ya ujauzito.

Wataalam kutoka hifadhi hiyo wanaamini kuwa mabaki hayo yalikuwa ya mwanamke wa hadhi ya juu kati umri wa miaka 20 na 30, aliyefariki dunia karne ya kwanza kabla ya kristo.

 

“Kinachooneshwa hapa ndio mfano pekee unaojulikana wa maiti ya kale ya mwanamke mjamzito,” makala katika jarida hilo imeandikwa ikitangaza utafiti wake.

 

Kwa kutumia urefu wa kichwa cha mtoto aliyekuwa tumboni, walikadiria alikuwa kati ya wiki 26 na 30 wakati mama yake anafariki dunia kwasababu ambazo hazikufahamika.

 

“Ni muhimu sana kufikia utafiti huu, unashangaza kweli,” mmoja wa timu hiyo Wojciech Ejsmond kutoka chuo cha Sayansi cha Uholanzi amezungumza na Shirika la Associated Press.

 

Wanasayansi walisema haikufahamika kwanini mtoto huyo hakuwa ametolewa tumboni lakini kilichoshukiwa kuchangia hilo ni imani juu ya maisha baada ya kifo au pengine kulikuwa na changamoto ya kufanya hivyo.

‘Mwanamke wa ajabu’

Watafiti wa maiti zilizohifadhiwa wameipa jina maiti hiyo, ‘Mwanamke wa ajabu’ kwasababu ya maelezo yanayokanganya kuhusu asili yake. Walisema kuwa mabaki ya maiti hiyo kwanza ilitolewa kwa chuo kikuu cha Warsaw mwaka 1826.

 

Aliyeitoa alidai kuwa maiti hiyo ilipatikana katika makaburi ya wafalme huko Thebes lakini watafiti wanasema karne ya 19 ilikuwa kawaida kutoa maelezo ya uongo kwa vitu vya kale katika maeneo maarufu ili kuongeza umaarufu wa sehemu hiyo.

 

Maandishi katika jeneza la jiwe yalikuwa chanzo cha wataalam karne ya 20 kuamini kuwa maiti iliyokuwa ndani ni ya kasisi wa kiume kwa jina Hor-Djehuti.

Lakini baada ya wanasayansi kugundua kuwa ni ya mwanamke mjamzito sasa wanaamini kwamba kuna wakati iliwekwa katika jeneza jingine kimakosa na wafanyabiashara wa zamani karne ya 19 kipindi uporaji na ufungaji tena wa mabaki ya kale ilikuwa jambo la kawaida.

 

Wameelezea hali ya maiti hiyo kuwa “iliyohifadhiwa vizuri” lakini imeharibiwa shingoni kwasababu ya kufunguliwa na kufungwa tena kukionesha kuwa kuna kipindi ilikuwa tunu inayolengwa.

 

Watalaam wanasema karibu vitu 15 vya kale ikiwemo talasimu zenye umbo la maiti zilipatikana ndani ya kifaa kilichotumiwa kufungia maiti.

Leave A Reply