MAITI YA MAMA YAKUTWA UFUKWENI

DAR ES SALAAM: Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Moza Hussein Lukanga, mkazi wa Mianzini Mbagala jijini Dar hivi karibuni mwili wake umekutwa ufukweni maeneo ya Bagamoyo akidaiwa kufa maji, Amani lina habari hii ya kusikitisha. 

 

Inaelezwa na chanzo chetu cha kuaminika kuwa, mwanamke huyo alitoka nyumbani kwake Aprili 25, mwaka huu, akiwa ameongozana na kijana aliyefahamika kwa jina la Juma akimtaka amsindikize sehemu ambayo hakuitaja awali.

 

“Huyu dada alikuwa na matatizo yake ya kiafya sasa siku hiyo alimuomba jirani yake aitwaye Juma amsindikize safari yake; wakatoka wote na inavyosemekana walikwenda Bagamoyo.

 

“Tukasubiri siku hiyo hakurudi, ilipofika jioni ikabidi tutoe taarifa kwa ndugu zake wakaja, tulipokuwa pale kuna watu walipiga simu kwa kaka wa marehemu na kusema maiti ya Moza imekutwa ufukweni. Hapo ndipo tulipochanganyikiwa, swali likawa imekuwaje akutwe amekufa, nani aliyemuua? Hatukupata majibu.

 

“Baadaye sana ndiyo tukaja kuambiwa kuwa, kumbe alifarikia dunia baada ya kuzama baharini kisha mwili wake kukutwa ufukweni,” alisema mtoa habari huyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini.

Akizungumza na Amani, kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Shazir Ally alisema alipigiwa simu na ndugu wa yule aliyemsindikiza (Juma) na kuambiwa kuwa mdogo wake amefariki dunia. “Siku ya tukio nilipigiwa simu na ndugu wa huyo kaka aliyemsindikiza kuwa Moza amekutwa amekufa ufukweni maeneo ya Bagamoyo.

 

“Ikabidi tukae hapa nyumbani ili kujua tunampataje huyo aliyemsindikiza na kujua mwili tutaupata sehemu gani. “Kwa bahati nzuri Juma ambaye aliondoka naye akawa amerudi na kutupa maelezo yake.

 

“Akasema marehemu alimuomba amsindikize safari yake, wakaenda mpaka Bagamoyo, walipofika kule wakaelekea baharini, walipokuwa pale marehemu alikwenda kunawa mikono kwenye maji, mawimbi yalipokuja yakamwingia mdomoni, akaanza kurukaruka, akajua amepandisha mashetani yake lakini haikuwa hivyo, akafariki baada ya kuzama baharini.

 

“Watu waliokuwa maeneo yale walipouona mwili huo ilibidi wamkamate yule kijana, wakampeleka polisi lakini baada ya kutoa maelezo akaachiwa, ndiyo amerudi na kuja kutuambia kuwa mwili upo Hospitali ya Bagamoyo, kwa hiyo tunaufuatilia ili tuweze kuuzika.

 

“Tukifanikiwa kuupata mwili tutazika katika makaburi ya Kongowe,” alimalizia kaka huyo wa marehemu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyegesa alisema kuwa, taarifa za kifo cha mwanamke huyo hazijamfikia na kuongeza kuwa huenda amekufa kifo cha kawaida ambacho hakuna aliyehusika.


Loading...

Toa comment