MAITI YACHUNWA NGOZI MOCHWARI

SISI hatuhusiki waulizeni wale! Ndivyo Jeshi la Polisi mkoani Singida na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wanavyotupiana mpira kutoa taarifa sahihi juu ya malalamiko ya baadhi ya ndugu wa marehemu, Amosi Mbua Muve wanaodai kuwa mwili wa ndugu yao ulichunwa ngozi na kunyofolewa baadhi ya viungo ukiwa umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo. 

 

Jambo la kukumbuka wanalodai ndugu hao ni kuwa wao waliupeleka mwili wa Muve kuhifadhiwa ukiwa salama na kwamba kilichotokea ni muujiza kwao.

 

Mmoja wa ndugu wa marehemu aitwaye Daudi Amosi Mbua ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu mkazi wa Kitongoji cha Mwacheche,Kijiji cha Mtamaa “A” alimwambia mwandishi wetu kuwa Agosti 26, mwaka huu saa mbili usiku baba yake alifariki katika Zahanati ya Kata Mwankoko alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

Alisema, baada ya kupewa taarifa hizo na mhudumu; familia walikubaliana kuupeleka mwili wa marehemu baba yake kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. “Agosti 27 tuliuchukua mwili wa baba hadi hospitali ya mkoa, wakati huo ulikuwa kamili, hakuna kiungo hata kimoja kilichokuwa kimepungua.

“Tulipofika chumba cha kuhifadhia maiti mwili ulipokelewa kwa taratibu zote, tukapewa kibali cha maandishi kwa makubaliano kwamba Agosti 29, tutakapokuja kuuchukua tuje nacho na kulipia gharama zote za kuhifadhia mwili huo,” alisisitiza mtoto huyo mkubwa wa marehemu.

TAARIFA YA KUSHITUA

Alisema katika hali ya kushangaza Agosti 29, mwaka huu walipokwenda kuuchukua mwili wa marehemu, mmoja kati ya wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti aliwaambia baadhi ya ndugu kuwa kuna taarifa mbaya kuhusu mwili wa ndugu yao ambayo hata yeye imemshangaza.

“Aliniambia nitafute wazee wawili au watatu tuongozane nao kwenda kuuona mwili wa baba; nikawatafuta. “Kusema kweli nilipata wasiwasi mkubwa lakini ikabidi kujikaza ili twende tukaone hicho ambacho mhudumu anasema hajakiona tangu azaliwe,” alisema mtoto huyo wa marehemu.

Aliongeza kuwa; walipoingia kwenye chumba cha kuhifadhia maiti walikuta mwili wa baba yake ukiwa umewekwa kwenye jokofu jambo ambalo mhudumu alilazimika kulifungua ili ndugu wajionee kile ambacho yeye hajakiona tangu azaliwe.

NGOZI, PUA, MDOMO, TITI VYANYOFOLEWA

“Nilipousogeza mwili wa baba ili tuuone nilipoutazama usoni niliona ngozi ya uso ikiwa imechunwa na kuondolewa sehemu ya nyama. “Sikuamini nilichokiona, hata wale wazee tuliokuwa nao walishangaa pia, lakini baadaye tulipozidi kukagua tukaona pua nayo imekatwa,”alisisitiza mtoto huyo wa marehemu.

Aidha, mtoto huyo mkubwa wa marehemu alivitaja viungo vingine vilivyonyofolewa kwenye mwili wa baba yake kuwa ni pamoja na mdomo wa juu na chuchu ya kulia. “Tukamuuliza huyo mhudumu ni nani ameufanyia unyama mwili wa baba yetu? Alishindwa kutupa jibu na kutuambia kuwa twende kwa katibu wa afya wa hospitali.”

MSIKIE MGANGA MFAWIDHI

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dk Deogratius Banuba licha ya kukiri kuwepo kwa tukio hilo, alikataa kuzungumzia chochote. “Kuhusu hatua zilizochukuliwa au zinazotarajiwa kuchukuliwa siwezi kusema kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi,” alisema Dk Banuba.

Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike pamoja na kukiri kuwepo kwa tukio hilo lakini akasema mwenye jukumu la kuongelea suala hilo ni mganga mkuu wa mkoa wa Singida na wala siyo jeshi la polisi.

“Kwa kweli taarifa za tukio hili ninazo lakini baada ya kuzipitia nimegundua kuwa anayetakiwa kulizungumzia tukio hilo ni mganga mkuu kwani marehemu alikufa kifo cha kawaida na kama angekuwa ameuawa au ni ajali ningehusika kikamilifu kulitolea maelezo,” alifafanua Kamanda Njewike.

Akiongea kwa njia ya simu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Victoriana Ludovic aliahidi kulizungumzia suala hilo atakaporejea kutoka safarini Dodoma na baada ya kulitafakari jambo hilo kwa kina.

NDUGU WAKABIDHIWA MWILI

Pamoja na kuwepo kwa tuhuma za mwili wa ndugu yao kuchunwa ngozi na kunyofolea baadhi ya viungo, ndugu wa marehemu walikabidhiwa mwili wakauzike wakati taratibu nyingine za kiuchunguzi zikiendelea.

Hadi tunakwenda mtamboni hakuna taarifa kutoka upande unaotuhumiwa wala kwenye mamlaka za dola ambao umeweza kutegua kitendawili cha nani alihusika na uhalifu huo na kwa sababu gani? Uwazi linaendelea kufuatilia skendo hii na kwamba litakapopata taarifa litawaletea kupitia vyombo vyake vya habari vikiwemo +255Global Radio, Global TV Online na magazeti.

Stori: Jumbe Ismailly, SINGIDA


Loading...

Toa comment