The House of Favourite Newspapers

Majaliwa Aagiza Kodi, Tozo za Mkonge Zifanyiwe Mapitio

0

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio ya kodi na tozo zote zilizopo katika zao la mkonge kwa lengo la kubaini ni zipi zenye manufaa kwa wadau na Taifa na kuainisha zisizokuwa na tija ili zifanyiwe mchakato wa kuondolewa.

 

Pia, Waziri Mkuu alizitaka taasisi za kifedha nchini ziendelee kuangalia kiasi cha riba kinachotozwa kwa wakulima wanaokopeshwa ili zisisababishe wahusika kushindwa kukopa kutokana na ukubwa wa riba.

 

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatano, Januari 20, 2021) wakati wa kikao chake na wadau wa mkonge kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga, ambapo alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kufuatilia mwenendo wa mazao yote ya biashara.

 

Alisema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha zao la mkonge linarudi katika nafasi yake, hivyo aliiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kuratibu maendeleo yake kuanzia hatua za utayarishaji mashamba hadi mwenendo wa masoko.

 

“Mkonge unafaida nyingi lakini sisi tumejikita katika utengenezaji wa nyuzi tu, tutumie wataalamu wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwa ajili ya kutumia fursa nyingine zinazopatikana katika zao hili kwa kutengeneza sukari, mbolea na vinywaji.”

 

Waziri Mkuu alisema Wizara ya Kilimo iendelee kukiboresha Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano na ijiridhishe kama kina vifaa vya kutosha katika uzalishaji wa miche ya mkonge. Pia aliiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania ishirikiane kikamilifu na kituo hicho ili kuendelea kuboresha zao hilo.

 

Leave A Reply