The House of Favourite Newspapers

Majaliwa Aipongeza GGML kwa Kuwainua Wanawake, Mhitimu FFT Aula

0
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Meneja (Utawala bora) fedha kutoka GGML, Tatu Tibashengwa cheti cha utambuzi wa mchango wa kampuni hiyo katika ufadhili wa mafunzo ya Mwanamke Kiongozi(Female Futura Tanzania-FFT) mwaka 2023. Tatu ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo yaliyofanyika kwa miezi tisa chini ya uratibu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE). Wengine waliohitimu kutoka GGML ni Changwa Mjella, Hellen Mallya na Flora Muhochi.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuwawezesha wanawake walioajiriwa ndani ya kampuni hiyo kujiendeleza kielimu pamoja na kuwapa promosheni za nafasi mbalimbali ikiwemo za uongozi pindi wanapohitimu mafunzo au masomo yao.

Pia ametoa wito kwa kampuni nyingine kutoa ufadhili wa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wanawake ili kuongeza tija katika matumizi ya kidijitali kama ilivyofanya GGML.

Majaliwa ametoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Tanzania) iliyoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti wakiwamo wahitimu wanne kutoka GGML.

Mmoja wa wahitimu hao ni Tatu Tibashengwa ambaye alikuwa Msimamizi wa Uthibiti wa Ndani,lakini hivi sasa amepandishwa cheo na kuwa Meneja (Utawala bora) fedha. Wengine waliohitimu kutoka GGML ni Changwa Mjella, Hellen Mallya na Flora Muhochi.

Akizungumzia hatua hiyo, Majaliwa alisema; “Nimefurahi kusikia wanawake kadhaa waliohitimu katika program hii wamefanikiwa kupata nafasi za juu za uongozi kama dada yetu wa GGML (Tatu Tibashengwa), hayo ndio mafanikio tunayoyataka.”

Aidha, alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika programu hiyo kwani imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa washiriki na kuleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wao wa kazi na kugusa maisha yao binafsi.

Pia aliwataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Tatu Tibashengwa (katikati) akiwa pamoja na wahitimu wengine katika mahafali ya nane ya mafunzo ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Tanzania – FFT) yanayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzani (ATE). Tatu baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya miezi tisa amepandishwa cheo kuwa Meneja (Utawala Bora) Fedha kutoka Msimamizi wa Udhibiti wa Ndani.

Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Doran alisema kuwa tangu waanze programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, wamekwishatoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo Wabunge na wawakilishi 150.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GGML, Terry Strong, Kaimu Meneja Rasilimali Watu, Dominic Marandu alisema tangu mafunzo hayo yalipoanzishwa mwaka 2016, GGML imepeleka jumla ya wafanyakazi wa kike 17 katika program ya kuwapatia mafunzo hayo ya Female Future Tanzania (FFT).

Alisema baadhi ya wahitimu wameteuliwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya kampuni hiyo, akiwemo mjumbe wa bodi ya STAMICO, Janeth Luponelo.

“Hivi sasa tupo katika mchakato wa kupendekeza majina ya wafanyakazi wengine wanne wa kike katika program inayofuatia,” alisema. Alisema GGML itaendelea kuongeza ujumuishwaji, usawa na kukubaliana na tofauti mbalimbali zilizopo katika makundi ya kijamii.

Akizungumzia promosheni aliyoipata kutoka GGML, Tatu Tibashengwa mbali na kueleza kuipokea kwa furaha, aliishukuru kampuni hiyo kwa kutambua utendaji wake uliotukuka, ufanisi, ujasiri na hata kudumisha dhana ya usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

“Ni sehemu ambayo wanawake wengine watavutiwa kufanya kazi na hata wenzangu walioajiriwa ndani ya kampuni, watapata hamasa ya kwamba inawezekana,” alisema.

Alisema ataitumia nafasi hiyo kuwawakilisha wanawake vizuri lakini pia atakuwa tayari kuwapa miongozo wanawake wanaotaka kuwa viongozi kama yeye.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply