Majaliwa: Anwani Za Makazi Kuchochea Ukuaji Wa Uchumi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mfumo wa anwani za makazi utasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi, kuharakisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama, kuwezesha biashara mtandao kufanyika kwa ufanisi na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 8, 2025) katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Katika kilele hicho Waziri Mkuu amezindua matumizi ya mfumo wa Anwani za Makazi. Kaulimbiu za maadhimisho hayo inasema “tambua na tumia anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma”.
Waziri Mkuu amesema suala la anwani za makazi ni moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022- 2025/2026 ambao umeweka bayana azma ya Serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi katika kata zote nchini.
“…siku kama ya leo tarehe 8 Februari, 2022, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini kwa njia ya operesheni. Operesheni hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi minne na kuwezesha ukusanyaji wa taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi zilizohifadhiwa katika mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi unaojulikana kwa jina la National Physical Addressing (NaPA).
Amesema kupitia programu ya NaPA mwananchi akiwa eneo lolote nchini na hujui sehemu ya kupata huduma za kijamii kama vile kituo cha afya au mgahawa anaweza kutumia programu hiyo kutafuta sehemu za karibu. “Hii ni programu bora na inarahisisha kupata huduma husika sambamba na kwenda na kasi ya kimaendeleo katika uchumi wa sasa wa Kijiditali.”
Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kutunza na kuwa walinzi wa miundombini ya anwani za makazi kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika kugharamia miradi hiyo. “Vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara, tunao Watanzania ambao si waaminifu wanang’oa mabago hayo na kwenda kuyauza, ni muhimu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa sababu inamanufaa.”