The House of Favourite Newspapers

Majaliwa: Rais Samia Ni Chachu ya Mapinduzi Katika Sekta ya Sanaa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejidhatiti kuendelea kukuza na kuimarisha sanaa nchini ikiwa ni moja ya sekta rasmi ya kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo Jumapili Aprili 13, 2025 katika Kongamano la Chama cha Wafawidhi wa Matukio Tanzania, linalofanyika Olasiti Garden, Mkoani Arusha. Ambapo amesema fani ya ushereheshaji ni uchumi.

Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia kaunzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambao unakopesha hadi shilingi Milioni 100 kwa wasanii wakiwemo washereheshaji ili waweze kujiimarisha kimitaji na vitendea kazi.

“Pia kupitia maboresho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999 yaliyofanyika mwaka 2022, Serikali imeanzishwa tozo ya hakimiliki (copyright levy) ambapo asilimia 60 ya makusanyo inakuja kwenu moja kwa moja na asilimia nyingine 10 inakuja kwenu kupitia Mfuko”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inatarajia kujenga Ukumbi wa Kimataifa ya Sanaa na Michezo ‘Arts and Sports Arena’ kwa shilingi bilioni 300. “Haya yote ni maono ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameaigiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kushirikiana chama cha Kisima cha Mafanikio katika kuandaa miongozo, mafunzo ya kitaaluma, na mfumo wa urasimishaji wa washereheshaji nchini.

“Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) endeleeni kushirikiana na Kisima cha Mafanikio katika kukuza matumizi sahihi ya Kiswahili kwenye majukwaa mbalimbali”.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inatambua kazi ya Chama cha Kisima cha Mafanikio. “Hakika kazi yenu ni ya msingi, nyeti na yenye mchango mkubwa kwa Taifa”.

Kwa Upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake mahiri na kwa kutoa fursa kwa watanzania kukuza vipaji vyao na kuendeleza stadi za kazi na taaluma katika tasnia mbalimbali ikiwemo ya ushereheshaji na upangaji wa matukio.