The House of Favourite Newspapers

Majaliwa, Ulega na Dkt. Tax Wakagua Miundombinu Iliyoathirika Somanga

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asubuhi Hii Aprili 16, 2025 amewasili eneo la Somanga kukagua Miundombinu ya barabara kuu ya Dar es Salaam-Lindi ambayo imeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stegomena Tax pamoja na Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega.

Aprili 06, 2025 wakala wa barabara Tanroad walitangaza kufunga kwa muda kwa barabara ya Somanga-Mtama baada ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha Wilayani Kilwa na hivyo kuharibu daraja la muda lililokuwa limejengwa eneo hilo ambapo baadae Wizara ya Ujenzi ilirejesha huduma za usafiri katika eneo hilo mara baada ya kujengwa kwa daraja la muda kuruhusu huduma za usafiri na usafirishaji kuendelea.

“Serikali baada ya mwaka jana kupatikana kwa tatizo la namna hii kuanzia muda huo ilifanya kazi muhimu ya kutafuta suluhu ya kudumu na suluhu ya kudumu ni kujenga madaraja na kwa barabara hii tu tuna madaraja zaidi ya matano. Kwa Lindi peke yake Mhe. Rais aliidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni 130 kwaajili ya kujenga madaraja yaliyokatika.”

“Hili daraja ambalo limekatika hapa ni la muda tu, daraja lake kamili kwasasa lipo asilimia 48 za ujenzi wake na nguzo takribani 27 kati ya 48 zenye urefu wa mita zaidi ya 12 zimeshasimikwa ardhini.” Alikaririwa Waziri Ulega wakati akisimamia ujenzi wa daraja hilo la muda.