The House of Favourite Newspapers

Majaliwa: Vifo Vitokanavyo na Ukimwi Vimepungua

0

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema uimarishaji wa huduma za tiba yakiwemo matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na ukimwi kutoka vifo 85,000 mwaka 2001 hadi kufikia vifo 21,529 mwaka 2019.

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Jumanne, Desemba Mosi, 2020, katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Mandela Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, ambapo kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Mshikamano wa Kimataifa, Tuwajibike Pamoja.’

 

Majaliwa amesema mbali na kupungua kwa vifo hivyo, pia maambukizi mapya nayo yamezidi kupungua kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi kufikia watu 68,484 mwaka 2019, hivyo ametoa wito kwa wadau wote katika mapambano ya ugonjwa huo waongeze jitihada.

 

“Mafanikio yote haya yametokana na kuendelea kuimarika kwa huduma za tiba yakiwemo matumizi ya (ARVs na hatua za kinga zinazohusisha tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” amesema.

 

Amesema Tanzania imefanikiwa kufikia malengo ya tisini tatu (90:90:90) hasa katika 90 ya pili na ya tatu.

 

“Kwa kujikumbusha tu, ni kwamba tisini tatu zinalenga kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya WAVIU wanajua hali zao; asilimia 90 ya wanaojua hali zao wanaanza kutumia dawa za kufubaza mapema na asilimia 90 ya walioanza dawa za kufubaza VVU kinga zao za mwili zinaimarika ifikapo mwaka 2023,” amsisitiza.

 

Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya mapambano dhidi ya VVU na ukimwi, waongeze jitihada hususani katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili wafikie lengo la 90 ya kwanza.

Leave A Reply