The House of Favourite Newspapers

Majaliwa: Waliozembea Ajali ya Moto Moro Wachukuliwe Hatua

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka husika ziwachukulie hatua za kinidhamu watu wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo kufuatia tukio la ajali ya moto iliyotokea Agosti 10, 2019, mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu 104, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali.

Ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma hadi tarehe 3, Novemba mwaka huu.

“Baada ya tukio hilo la kusikitisha tarehe 12 Agosti 2019 niliunda kamati maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

“Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea,” alisema.

Alitumia pia fursa hiyo kuwashukuru madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wadau wote ambao walishiriki kuokoa maisha ya waathirika wa ajali hiyo tangu ilipotokea.

“Nawasihi Watanzania wenzangu tujifunze kutokana na ajali hiyo iliyotokea Morogoro na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika maeneo ya ajali. Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada kwa waathirika wa ajali badala ya kutumia kama fursa za kujinufaisha isivyo halali,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.

Comments are closed.