JESHI la Polisi Mkoa wa Geita limefanikiwa kuwakamata watu sita wanaosadikika kuwa ni majambazi waliotekeleza tukio la mauaji ya Betrice Silvanusy (29), mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Ibolelo, kata ya Nyankumbu wilayani Geita Mkoani hapa siku ya aprili 27 mwaka huu.
Akitoa taarifa hiyo jana mbele ya waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (ACP) Henry Mwaibambe aliwataja watuhumiwa hao ni Yasini Zuberi (36), Khasimu Marwa (39), Leonard Emmanuel (34), Fikiri Ezekieli (31), Thomas Daniel (29) na Samson Charles (30) wote wakazi wa wilaya ya Geita.
ACP Mwaibambe alisema baada ya tukio kutokea jeshi la pollisi lilifanya upelelezi wa kina na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na simu ya marehemu na wamekiri kugawana fedha kiasi cha shilingi 1,500,000/= ambayo walimpora marehemu.
Kamanda wa Polisi alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na watuhumiwa walifikishwa mahakamani jana na kusomewa shitaka la mauaji namba 19/2021 katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Geita.
Ikumbukwe, mapema mwezi huu jeshi la polisi mkoani hapa lilithibitisha kutokea kwa mauaji ya mfanyabiashara huyo yaliyotokea usiku wa aprili 27 mwaka huu majira ya saa nne usiku wakati marehemu akiwa anatokea kwenye shughuli zake za biashara kurejea nyumbani.
Jeshi la polisi lilieleza, wakati marehemu akiwa kwenye usafiri wa bajaji alivamiwa na kundi la majambazi zaidi ya watano na kumpiga na kitu kizito kichwani na kupelekea umauti wake ambapo walimupora simu na fedha alizokuwa nazo.