The House of Favourite Newspapers

Majambazi Yamponza Kigogo wa Polisi

0

MAJAMBAZI yaliyomvamia mfanyabiashara mmoja, Mkombozi Mjaila (32) wilayani Handeni, mkoani Tanga na kumjeruhi kichwani, yamemponza kigogo wa polisi ambaye ni mkuu wa kituo, kwani ameng’olewa katika kituo hicho.

 

Mkuu huyo wa Kituo cha Polisi cha Mnubi, aliyefahamika kwa jina moja la Konki, alimkasirisha Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Toba Nguvila aliyetembelea eneo la tukio na kuamuru Mkuu wa Polisi wilayani humo (OCD), Willium Nyelu, kumhamisha Konki pamoja na askari wengine waliokuwa zamu siku ya tukio ndani ya siku saba.

 

“OCD nakuagiza kumuondoa mkuu wa kituo hiki (Konki) ndani ya siku saba na ikiwezekana hata kesho asionekane hapa, mwambie mkubwa wako huyu mtu sitaki kumuona kwenye wilaya yangu, na hao askari waliokuwa zamu siku hiyo, uwaondoe hapa uwapeleke wilayani na utoe wengine wenye nidhamu kule wilayani uwalete hapa,” aliamuru mkuu huyo wa wilaya.

 

Aidha, alimuelezea Konki kuwa ni askari asiyekuwa na nidhamu ya kazi, kwani analalamikiwa kwa rushwa na kuwadhulumu wafanyabiashara kwenye mji huo ambapo wananchi wamekuwa wakitoa malalamiko yao kituoni hapo, lakini hakuwa akiwatetea wala kuwajali akiwa kama kiongozi wa polisi.

 

Mjaila alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao walimjeruhi kichwani kwa kitu chenye ncha kali, kisha kumpora pesa taslimu shilingi milioni saba pamoja na simu za mkononi zaidi ya 25 alizokuwa akiziuza.

 

Majeruhi huyo mkazi wa mtaa wa Kulimba A katika Kata ya Mkata, wilayani Handeni, alipelekwa Kituo cha Afya cha Mkata kwa matibabu na akasema kuwa alipatwa na mkasa huo usiku wa saa nane kuamkia Ijumaa iliyopita.

 

Akisimulia mkasa huo, Mjaila ambaye anafanya biashara ya duka la spea, duka la simu za mkononi na vifaa vyake pamoja na duka la uwakala wa miamala ya pesa mitandao yote ya simu, alisema kwamba, usiku wa tukio, alisikia geti likifunguliwa kwa kupigwa na vitu vizito kabla watu hao hawajaufikia mlango wa kuingilia ndani, aliamka kuuendea mlango, lakini kabla hajaufikia, alishtuka mlango huo umefunguliwa kwa kupigwa na kitu kizito.

 

“Niliuendea mlango nikausukuma kwa nje, lakini ukarudishwa tena ndani na watu watatu wakaingia huku wakitaka niwape pesa, kabla sijajibu, mmoja akanipiga na kitu kama jembe lenye mpini mfupi, usoni, nikajikuta nikitiririkwa na damu.

 

“Baada ya dakika chache, majambazi wengine walimgeukia mke wangu na kuanza kumpiga, walichukua simu zetu mbili, wakachukua na simu tano za ofisi za kurushia miamala pamoja na pesa taslimu shilingi milioni saba ambazo zilikuwa mauzo ya siku hiyo,” alisema Mjaila.

 

Majeruhi huyo alisema wahalifu hao walijigawa kwenye makundi tofauti na kila kundi la watu watatu lilivamia nyumba za watu kwa wakati tofauti kwa kuvunja milango na kuwapiga watu, huku wakidai pesa.

 

Katika tukio hilo, pia watu wengine ambao walikuwa majirani wa Mjaila, walifanikiwa kupiga simu kituo cha polisi lakini hawakuweza kupata msaada wa haraka, jambo lililomtibua mkuu wa wilaya.

STORI: ELVAN STAMBULI, DAR

Leave A Reply