Majembe Saba Yaipa Kicheko Simba Katika Orodha ya Kuwania Tuzo
MAJEMBE saba yanayovuja jasho la haki ndani ya kikosi cha Simba yamewapa kicheko Simba wakiamini kuwa hawajabahatisha kupenya kwenye orodha ya kuwania tuzo bali ubora umewababe.
Katika orodha ya kuwania tuzo ndani ya ligi msimu wa 2022/23 tayari Kamati ya Tuzo Tanzania iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imetaja mastaa waliopenya kuwania tuzo zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni huku Simba ikitoa mastaa saba.
Ni kwenye kipengele cha mchezaji bora ni nyota wawili wamepenya ambao ni Mzamiru Yassin na Saido Ntibanzokiza wote ni viungo.
Aishi Manula maarufu kama Air Manula kipa namba moja wa timu hiyo amepenya kwenye kuwania tuzo ya kipa bora akipambana na Djigui Diarra wa Yanga na Benedict Haule wa Singida Big Stars.
Watatu wamepenya kwenye tuzo ya beki bora ambao ni Shomari Kapombe, Henock Inonga na Mohamed Hussein sawa na watatu waliopenya kuwania tuzo ya kiungo bora ikiwa ni Clatous Chama, Mzamiru na Sadio.
Wakati wachezaji wao wakipenya na jina la kocha Roberto Oliveira nalo limetajwa kwenye kipengele cha kuwania tuzo ya kocha bora msimu wa 2022/23.
Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa hilo ni jambo kubwa na linadhihirisha ubora walionao.
“Wachezaji wa Simba kutajwa kwenye orodha ya kuwania tuzo ni jambo linamaanisha kuwa kikosi kina wachezaji bora na wengi wametajwa kuwania tuzo hivyo mambo mazuri yanakuja.”
Stori: Lunyamadzo Mlyuka