The House of Favourite Newspapers

Majembe ya Kaskazini Yanayofanya Maajabu

0

KILA afanyaye kazi mwisho wa siku hutarajia mafanikio katika kile anachokifanya, hii inaleta tathimini ya kujua wapi kakosea, nini aongeze na kipi akipunguze.

 

Maana yangu ni kwamba, katika tasnia ya burudani hapa Bongo, imekuwa ikileta mafanikio kwa baadhi ya wasanii kutokana na kazi zao wanazofanya.

Makala haya yanakuletea watu maarufu kutoka Nyanda za Kaskazini ambao wamefanya ‘wandaz’ hapa Bongo.

 

WEUSI

Hili ni kundi kutoka Kanda ya Kaskazini ambalo linajumuisha wanamuziki watano wote wakiwa wanatokea Arusha.

Wanamuziki hao ni Joh Makini, Niki wa Pili, G Nako, Lord Eyez pamoja na Bonta Maarifa.

 

Hili ni kundi maarufu la wanamuziki wa Hip Hop hapa nchini na wamekuwa wakifanya maajabu wanapokuwa stejini. Shoo zao zimekuwa zikijaza watu sana kitendo cha kufanya watu waamini kuwa, ndani yao kuna maajabu ya kutosha kwani wamekuwa wakitoa ngoma kali kama Ni Come, Gere, Madaraka Ya Kulevya, Wapoloo, Swagiree na Showtime.

 

VEE MONEY

Unaweza ukamuita pia Cash Madame, majina ambayo yameendana na hadhi yake kutokana na kujituma kwake. Ni mwandishi, muimbaji, pia ni Mtangazaji. Vanessa amewahi kutamba na vibao kama Nobody But Me, Cash Madame, Kisela, Bambino na nyingine nyingi ambazo zilimtangaza ndani na nje ya nchi.

 

DOGO JANJA

Abdulazizi Chende ni moja kati ya wasanii waliokuja Bongo wakiwa na umri mdogo sana, lakini akiwa kwenye Kundi la Tip Top Connection chini ya Madee.

Ngoma zilizompa umaarufu ni kama Banana, Yente, Wayu Wayu, Ukivaaje Unapendeza pamoja na nyingine nyingi.

 

NANDY

Faustina Charles Mfinanga ni muimbaji, mtunzi, pia ana kipaji cha kubuni na kushona mavazi kwani ana kampuni yake ya kutengeneza nguo za asili ijulikanayo kama The African Princess Print. Nandy anatamba na vibao kama Nagusagusa, One Day, Kivuruge, Haleluyah, Hazipo, Aibu na vingine kibao.

Mwanadada huyu amejipatia mafanikio kwa kasi ya ajabu kupitia kazi zake maana anamiliki mjengo na magari ya kifahari.

 

ELIZABETH MICHAEL

Lulu ni mmoja kati ya wasichana wenye umri mdogo ambao wanapambana. Kama unakumbuka mwanadada huyu alianzia kuigiza Kaole Sanaa Group na alipata bahati ya kuigiza na wasanii wakubwa hapa bongo akiwemo Marehemu Steven Kanumba na wengine wengi na kulifanya jina lake kuwa kubwa.

 

BARNABA CLASSIC

Elias Barnabas ni moja ya wasanii wakongwe wasiochuja katika kazi zao. Ametamba na ngoma kama Sichomoi, Tunafanana, Lover Boy, Magumegume, Njia Panda na nyingine nyingi, amekuwa akifanya maajabu akiwa stejini na kukusanya mashabiki kama kijiji katika shoo zake.

 

WHOZU

Amepata umaarufu sana katika uigizaji wa vichekesho na baadaye alipobipu tu kwenye Bongo Fleva, hapo ndipo alijulikana mazima na wimbo wake wa Hauendi Mbinguni, Roboti na nyingine nyingi.

Whozu kwa sasa amekuwa na maendeleo makubwa kwani amefungua duka lake la nguo linalojulikana kwa jina la Whozu Empire.

 

JACQUELINE WOLPER

Mwanadada huyu ni miongoni mwa wanawake wanaojituma sana na amepata umaarufu mkubwa hapa Bongo kupitia fani ya uigizaji.

Katika filamu mbalimbali ikiwemo Red Valentine, Tom Boy, Mahaba Niue na nyingine, Wolper alifunika mbaya.

Ukiachilia mbali kazi ya uigizaji, mwanadada huyu ni mwanamitindo na mjasiriamali ambaye anamiliki kampuni ya ubunifu ya mavazi inayojulikana kwa jina la Wolperstylish ambapo kazi hii imemfanya Wolper kusafiri maeneo tofauti ndani na nje ya nchi kutokana na biashara yake.

 

NAHREEL

Jina alilopewa na wazazi wake ni Emmanuel Mkono, watu wengi wanamfahamu kama Nahreel. Ni mtayarishaji wa muziki na ametengeneza kazi nyingi za wasanii mbalimbali ambazo zimekuwa moto wa kuotea mbali, ngoma kibao za wasanii kama Weusi, Vanessa na wengine wengi. Mbali na hilo, Nahreel ni prodyuza, pia anaimba na amefanikiwa kutengeneza ngoma kali akiwa na mpenzi wake Aika, na kati ya maprodyuza walio na mafanikio makubwa kupitia kazi zao lazima umtaje Nahreel maana anamiliki mjengo wa maana na studio yake mwenyewe inayojulikana kama The Industry.

 

ROSA REE

Katika marapa wanaojulikana nchini Tanzania, huwezi acha kumtaja mwanadada Rosary Robert ‘Rosa Ree’. Huyu ni mwamba wa kike anayefanya maajabu hapa Bongo.

 

Amepata umaarufu mkubwa kutokana na staili yake ya uimbaji wa kurapu kwa kutumia Kiingereza.

Kwa hapa Tanzania ni wanawake wachache sana wanaojua kuchana hivyo. Rosa Ree ana ngoma kama Banjuka, Nguvu za Kiume na nyingine nyingi.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI

Leave A Reply