Majeraha ya Yacouba Pasua Kichwa Yanga

MAJERAHA ya nyama za paja aliyoyapata kiungo mshambuliaji nyota wa Yanga, Yacouba Songne yameendelea kukiweka kikosi hicho katika hofu kubwa ya kumkosa nyota huyo kwa muda mrefu.
Yacouba aliyehusika kwenye mabao nane ya Yanga akifunga mabao manne na kuasisti mara nne, alipata majeraha hayo kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC, na kumfanya akosekane kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Simba uliopigwa, juzi Jumatano.
Kwenye fainali hiyo Yanga waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Simba kwa mikwaju ya penalti 4-3, walitwaa taji hilo kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwa kombe hilo rasmi mwaka 2007.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja wa kikosi cha Yanga, Hafi dh Saleh, alisema nyota huyo bado anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, na anatarajiwa kufanyiwa vipimo tena ili kujiridhisha juu ya hali yake.
“Yacouba bado anasumbuliwa na majeraha ya nyama za paja, hapo mwanzo tulitarajia angekuwa sehemu ya mchezo wa fainali dhidi ya Simba siku ya Jumatano lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo.“
Hii ni baada ya madaktari kuamuru aendelee kupata mapumziko na atafanyiwa tena vipimo ili kujiridhisha juu ya maendeleo yake,” alisema Saleh.Kuhusu safari ya kurejea kwao jijini Dar es Salaam, Saleh alisema: “Kikosi chetu kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho (leo) Ijumaa ambapo taratibu nyingine za mapumziko zitafuata, kabla ya kurejea kambini.”

