Meya wa Jiji la Brovary lilipo nchini Ukraine, Ihor Sapozhko kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook amethibitisha kifo cha aliyekuwa katibu wa jiji hilo Oleksiy Zdorovets.
Sapozhko amenukuliwa akisema aligundua kuwa katibu huyo wa zamani wa jiji, alifariki dunia wakati wapiganaji wa Urusi walipovamia na kulikama Jiji la Nova Bohadanivka ambako ndipo alipokuwa akiishi yeye na familia yake akiwemo mke na mtoto wao wa kiume.
Meya Sapozhko ameandika: “Habari mbaya ya kifo cha Oleksiy Zdorovets, katibu wa zamani wa Jiji la Brovary ambaye aliuawa na wapiganaji wa Urusi, imetufikia leo.”
Ameendelea kwa kusema: “Wanayofanya wanajeshi wa Urusi katika ardhi yetu ni uhalifu dhidi ya haki za binadamu, kwa niaba ya Jiji la Brovary pamoja na kamati kuu natuma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu wa marehemu lakini pia kwa niaba yangu na kwa niaba ya kila mmoja ambaye alikuwa anamjua Oleksiy.”
Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov amesema kuwa mpaka kufikia Machi 10, 2022 idadi ya raia waliouawa na wanajeshi wa Urusi ilizidi idadi ya ngome zote za wanajeshi wa Ukraine waliofariki katika mapigano.
Vita kati ya Urusi na Ukraine bado vinaendelea kupamba moto huku kukiwa na juhudi mbalimbali za kuhakikisha vita hivyo vinamalizika ili kuokoa maisha ya raia wengi wasiokuwa na hatia.