BAADHI ya wachezaji na viongozi wa timu ya Majimaji FC ya Songea Ruvuma, mapema leo walipata fursa ya kutembelea ofisi za wadhamini wao wakuu, kampuni ya mchezo wa kubashiri ya SOKABET zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam.
Viongozi na wachezaji hao waliamua kutumia muda wao wa mapumziko ya wiki moja kutembelea na kuona namna ofisi za wadhamini wao zinavyojiendesha kwa kutoa huduma ya mchezo wa kubashiri kiasi cha kuwa na uwezo wa kuwadhamini.
Akizungumza ndani ya ofisi hizo, msemaji wa klabu hiyo, Onesmo Nduguru, alisema waliamua kutumia siku ya leo kuwatembelea wadhamini wao hao baada ya kutoka kushiriki katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting uliyochezwa Jumamosi iliyopita huku wakipoteza kwa bao 2-1.
“Klabu yetu ya Majimaji leo imeanza mapumziko ya muda wa wiki moja, hivyo tumeona ni vizuri tukatumia nafasi yetu ya leo kuwatembelea wadhamini wetu SOKABET kabla hatujasambaa kabisa kwani tayari kambi tumeshaivunja na kuwataka wachezaji kila mmoja atumie muda huu kufanya mambo yake ila hawa wachache tumeona ni vyema tuje nao kutembelea hapa,” alisema Ndunguru.
HABARI/PICHA: MUSA MATEJA/GLOBALPUBLISHERS