MAJIZO AWAKA, KISA LULU

WAKATI ukimya ukiwa umetawala kwa muda tangu kutangazwa kwa ndoa yao huku maneno yakiwa mengi kuwa harusi yake na mwigizaji mkali wa Bongo Movies, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ imeyeyuka, mmiliki wa Kituo cha Redio cha EFM na Televisheni ya TVE, Francis Anthony Ciza ‘DJ Majizzo’ amewaka ile mbaya.

 

Mwishoni mwa mwaka jana, picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Majizzo akimvisha pete ya uchumba Lulu, jambo ambalo liliamsha shangwe kwa mashabiki wengi mtandaoni waliokuwa wakiipenda kapo hiyo.

 

 

Katika tukio hilo lililofanyika nyumbani kwa Majizzo, Mbezi-Beach jijini Dar na kushereheshwa na mwigizaji wa Bongo Movies, Mahsein  Awadhi Said ‘Dk Cheni’, Lulu alishindwa kujizuia hisia zake za kuvalishwa pete hiyo kwa kuangua kilio.

Hata hivyo, wiki chache mbele, Lulu alidaiwa kuvua pete hiyo baada ya kudaiwa kukorofishana na jamaa huyo huku akionesha kujiachia peke yake sehemu mbalimbali ikiwemo katika hifadhi ya wanyama ya Serengeti na maneno yakizuka upya mitandaoni kuwa hakuna tena ndoa kati yao.

Wakati yote hayo yanaendelea, mapema wiki hii Majizzo alifanyiwa mahojiano na Kipindi cha Genge cha Radio EFM ambapo aliulizwa juu ya maneno hayo yanayosambaa mitandaoni kuhusiana na ndoa yake.

“Watu wa mitandaoni hawanijui hata huyu binti (Lulu) hawamjui, kwa kuwasaidia tu waachane na sisi maisha yao yatakuwa rahisi,” alisema Majizzo muda mfupi kabla ya kutambulisha wimbo wake mpya wa Singeli redioni hapo.

Wawili hao wanadaiwa kuanza uhusiano tangu mwaka 2016 ambapo kabla ya hapo, Majizzo alikuwa na uhusiano na mwanamitindo Hamisa Mobeto na kufanikiwa kuzaa naye mtoto mmoja wa kike. Uhusiano wake na Lulu ulikua kwa kasi zaidi mwaka jana baada ya mrembo huyo kumaliza adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili jela kwa kukutwa na hatia na mahakama ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa staa wa filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba.


Loading...

Toa comment