Majuto arejea toka Makka shavu dodo!

Staa wa filamu za Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ alipowasili toka kuhiji Makka.

Gladness Mallya na Hamida Hassan

MABADILIKO! Baada ya kunusurika kwenye vifo vya mkanyagano vilivyoua mahujaji zaidi ya 4000 waliokwenda kuhiji katika mji wa Mina, Makka nchini Saudi Arabia, staa wa filamu za Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ amerejea salama akiwa shavu dodo na kusema ameachana na maisha ya zamani, sasa amekuwa mtu wa tofauti kabisa.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko katika mahojiano maalum mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jumamosi iliyopita na kupokewa kifalme, kwani mamia ya ndugu waliofika uwanjani hapo kuwapokea mahujaji wengine, walitaka kumpa mkono na kupiga picha na staa huyo wa vichekesho nchini .

….Akipokelewa na ndugu zake.

SANAA BASI?

Alisema: “Nimerudi salama jamani. Lakini nimejifunza mengi sana kule Makka. Tamko langu kubwa kuhusu sanaa ni kwamba, sitacheza tena filamu zinazohusu mapenzimapenzi wala kushiriki matangazo ya kwenye runinga yenye mwelekeo wa mapenzi. Sitaingia tena baa. Pia masuala ya wasichana ‘dogodogo’ ambao wamezoea kunishobokea wanatakiwa wapite mbali na mimi.

“Lakini pia kuna hii tabia ya wasichana kutaka kupiga picha na mimi kwa kutumia simu za Smart Phone, wenyewe mnaita ‘selfie’ sitaki kwani mambo yote hayo ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu na yatanirudisha nilikokuwa zamani, sitaki nitoke kwenye maisha yangu ya sasa yaliyobaki hapa duniani.”

AWEKA KIAPO

Mzee Majuto alikwenda mbele zaidi kwa kusema kwa sasa ataishi maisha ya kitakatifu zaidi, ambapo kwa mwezi atatumia siku kumi kusafiri sehemu mbalimbali za nchi kwa ajili ya kuwafundisha watu mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

“Ukweli sasa nimekuwa mtu wa ibada kila mara. Kama ni filamu nitacheza zile ambazo hazimchukizi Mwenyezi Mungu. Na muda mwingi nitawafundisha watu mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Nikiona sanaa inaniingiza majaribuni nitaachana nayo kabisa kwani tayari nimeshajenga msikiti na madrasa kule Tanga,” alisema Mzee Majuto.

AOMBA AOMBEWE

Alisema: “Mimi ni binadamu, hivyo kwa nguvu zangu na akili zangu sitaweza kuyatimiza hayo, hivyo nawaomba Watanzania waniombee ili niishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na nisirudi kule nilikokuwa zamani.”

ALIVYONUSURIKA KUFA MAKKA
Aidha, Mzee Majuto alianika jinsi yeye na mahujaji wengine walivyofanikiwa kumaliza ibada ya hija salama Makka na mahujaji wote wakaelekea kwenye kutimiza nguzo tano za Kiislamu za kumpiga mawe shetani Mina ambako huko ndiko maafa ya kukanyagana yalitokea.

Alisema: “Nilikuwa tayari kwenda Mina lakini kilichoninusuru nisiende, mimi nina tatizo la goti hivyo kwenda huko nilishindwa, nikamuomba mtu akanisaidie kunirushia jiwe langu la kumpiga shetani, mimi nikabaki hotelini. Lakini baada ya muda mfupi alirudi na kuniambia hali ni mbaya na mahujaji wengi wamekufa kwa kukanyagana.
“Ila kwa unene wangu huu, naamini kama ningekuwa miongoni mwa watu waliokwenda Mina kumpiga shetani, huenda ningekanyagwa na kufa.”

ILIKUWAJE?

Kwa mujibu wa Mzee Majuto, vifo hivyo vilitokea kwa sababu ya kufungwa kwa njia moja kati ya mbili za kuingilia Mina kutokana na matumizi ya kifalme, ikabidi itumike njia moja kinyume na utaratibu ambapo idadi ya mahujaji waliokuwa wanakwenda na wanaorudi ilikuwa kubwa.

Loading...

Toa comment