Makaburini Ndipo Walipolala Wenye Utajiri Mkubwa!
KUZALIWA na kuishi duniani ni kutimiza kusudio la Mungu. Lipo kusudi ambalo Mungu analitaka ulitimize katika dunia hii nzuri yenye vitu vizuri vilivyoumbwa na Mungu. Hivyo ipo sababu ambayo ipo mbele za Mungu aliyokupa wewe uzaliwe mahali ulipo.
Wengi wetu tumezaliwa tukiwa na vipaji vingi na wenye uwezo mkubwa, lakini mara nyingi nimesema kuwa wapo walioondoka katika ulimwengu huu bila ya wao kufahamu uwezo uliopo ndani yao.
Kutokana na hali ya kutojitambua, imewafanya kuhakiki ule usemi; “Makaburini ndipo mahali walipolala watu wenye utajiri mkubwa.” Utajiri ambao walipokuwa hai hawakuujua wala kuutambua uwezo wao ambao kama wangeutambua, basi leo hii ulimwengu ungekuwa ukishuhudia maajabu chanya kwa waliyoyafanya. Hivyo basi, kuondoka duniani bila kutimiza kusudio na wajibu wako kwa jamii yako ni kitu kibaya mno.
Leo nitakupa vitu muhimu vya kuzingatia ili ufikie mafanikio yako unayoyatamani;
Kila jambo lenye misingi katika ulimwengu huu hufungamanishwa katika misingi muhimu. Ipo misingi ambayo ukiifuata na kuifanya itakupeleka kwenye kilindi cha mafanikio na hutakwenda kulala kaburini na utajiri wako. Mambo yafuatayo tukiyatilia maanani, basi tutafanikiwa;
1: KUJITAMBUA (SELF DISCOVERY)
Kujitambua huja baada ya kujichunguza. Maisha ya mwanadamu hukamilika pale mwanadamu huyo kama atakuwa na tabia ya kujichunguza. Utambuzi binafsi husaidia mtu kujielewa kuwa yeye, wewe au mimi ni nani? Utambuzi binafsi wa mtu ni silaha kwa mtu mwenyewe ambayo humlinda mtu huyo dhidi ya tabiri zenye kukatisha tamaa kutoka kwa watu ambao wapo kwa ajili ya kuwakatisha tamaa wengine.
Mfano; utawasikia wakikueleza; “Huwezi kufanikiwa kwa sababu katika familia yenu hamna aliyefanikiwa.” Kitu muhimu cha kuweza kukabiliana na kauli za kukupuuza na kauli hasi za watu wa namna hii ni kujitambua. Daima elewa; “Dunia imejaa watu weledi wa kukosoa na kukatisha tamaa wenzao kila wanapoinuka. Usiwajali! Inuka na kuanza sasa!”
2: KANUNI
Tambua kuwa; “Daima maisha ni kanuni.” Kanuni ambazo ukizitumia lazima uelekee katika mafanikio. Kanuni hizi hutumiwa pia na waliofanikiwa daima nikiwemo mimi.
Hebu chunguza mfano huu; Taarifa (Information) + Kufanya Kazi = Mafanikio!
Hivyo, chochote unachokisikia au kuzungumzwa ni taarifa. Taarifa ambazo ukizitumia lazima mabadiliko uyaone. Kanuni hizi si mpya bali tunazo katika maisha yetu ya kila siku.
Hujulikana kama SHERIA ZA MAFANIKIO.
Kanuni hizi ni za kweli. Nizungumzacho ni kweli kwa maana mahali hapa nilipo kuna watu wanaonijua, wanaoijua familia yangu siku za nyuma enzi za uchumi mbaya.
Niliamua kuzitumia kanuni hizi kwa kufanya maagizo (taarifa), hakika nimeyashuhudia na ninaendelea kushuhudia mabadiliko katika maisha yangu na familia yangu kwa jumla. Nami leo kwa kulitimiza kusudi la Mungu ninasimama mbele yenu kuwaeleza kuwa jamii yetu inahitaji watu waliofanikiwa.
Haitafaa kitu katika nchi hii watu wachache wafanikiwe ilihali wengi wao hawakufanikiwa. Ili nchi yetu (Tanzania) iweze kuendelea katika nyanja kiuchumi na kijamii, tabaka la kati lazima lifanikiwe. Lazima liwe na uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao utawezesha watu wengine kuajiriwa na kununua pia.
Hivyo, nchi uliyopo ndiyo mahali sahihi kwako kufanikiwa. Unachopaswa kutenda ni wewe kujiamini. Kujiamini ni silaha katika kuelekea mafanikio. Kujiamini daima huleta mafanikio ambayo huanzia chini na si juu. Unapojiamini na kujenga hasira ya mafanikio ndani yako kuwa kwa nini yule alifanikiwa na mimi au wewe ushindwe. Kwa hiyo, kujiamini ni silaha ya kukupeleka katika mafanikio.
Tambua kuwa mtu awapo katika umaskini hupoteza kujiamini. Mfano halisi ni mimi, nikiwa darasa la tatu wenzangu walikuwa wakiniita mjinga wa darasa. Hivyo, kutokana na umaskini ambao familia yetu ilipitia, basi ulininyang’anya hali yangu ya kujiamini darasani na hata nje ya darasa. Umaskini wa familia yetu ulinisababisha jina langu kupotea na kupewa jina la Madaso ambalo ni jina la Kisukuma lenye maana ya mtu mwenye kuvaa nguo zilizochanika.
Umaskini ulinidhalilisha, ulisababisha nipuuzwe mimi na wazazi wangu. Siku moja nikiwa na umri wa miaka kumi na minne nilikwenda kwa mara ya kwanza katika msiba wa rafiki yangu ndipo niliposhuhudia wazazi wangu wakidhalilika kwa kukaa chini huku watoto wadogo wakiketi katika viti.
Nakumbuka wazazi wangu walinifundisha kuwa kila nimuonapo mtu mkubwa amesimama nami nimeketi katika kiti au kigoda ni lazima nimpishe. Hali ile ilinitia uchungu moyoni, nilimuuliza mama tukiwa nyumbani. Nililia mno kwa dharau ile kwa wazazi wangu.
Mama alininyamazisha kwa sala ya baraka katika maisha yangu. Jifunzeni kuwafunza watoto wenu adabu njema. Hivyo, mambo hayo yalinitia hasira ya mafanikio kwa kauli za ndani yangu kuwa; “Nitamfanya kila mtu kuwa na adabu kwa wazazi wangu.”
3: KUWA NA UPENDO WA DHATI
Upendo ni nguzo kuu katika maisha. Kuwa na upendo kwa watu wote, nchi yako na uudhihirishe upendo wako. Usiwe na kisasi kwani kisasi ni cha Mungu. Kwani kawaida ya Mungu kuwaleta mbele yako wale wote waliokutenda vibaya baada ya kufanikiwa ili uamue kuwasamehe au la.
Nakumbuka kijana mmoja aliwahi kufukuzwa kazi na mkuu wake kwa fitina ambayo ilitokana na utendaji kazi mzuri na elimu aliyokuwa nayo yule kijana. Hivyo, mkuu huyo alimfukuza kazi kijana yule kwa dhihaka na matusi. Baada ya miaka kadhaa kupita naye alifukuzwa kazi, akaanza kutafuta ofisi ya kukodi ili afungue ofisi yake.
Siku moja alijikuta katika jengo refu ambalo alikuwa akimuuliza secretary mara kijana yule aliyemfukuza alipita na akamuona kijana akipita. Alimuuliza huyu ni nani hapa? (kwa jazba) alimjibu kwa upole; “Huyu ndiye mkuu hapa na ndiye mwenye jengo hili”. Jamaa aliingia ofisini mikono ameweka nyuma, alikwenda kumtaka radhi na kumwambia; “Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.” Hivyo, upendo kwa watu wote ni mojawapo ya njia katika mafanikio.
4: JIVUNIE KITU ULICHONACHO
Mtu bora katika dunia hii ni yule anayekionea fahari kitu alichonacho hata kama ni kikubwa au kidogo.
Tambua kuwa mafanikio yako katika maisha yatatokana na hasira ya kufanikiwa, hivyo mateso au vitu ulivyopitia ndiyo nguvu itakayokusukuma kubadili maisha yako.
Pia amini kuwa Mungu hashindwi kukuinua. Elewa kuwa Mungu anapomnyanyua mtu, anamnyanyua kwa makusudi yake si kwa sababu wewe au mtu huyo ni mwema, la hasha! Ni kwa sababu tu Mungu wetu ni mwema na ni mwaminifu.
Itaendelea wiki ijayo.
NA ERIC SHIGONGO | BE INSPIRED & CHANGE
Comments are closed.