The House of Favourite Newspapers

Makalla Afunguka Kuhusu Barabara ya Buchosa Sengerema, “Mkandarasi Alishindwa Kazi”

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewahakikishia wakazi wa kata za Nyehunge na Bukokwa katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza kupitia Serikali kuwa itaanza kujenga barabara ya Buchosa hadi Sengerema kwa kiwango cha lami baada ya kupata mkandarasi mpya ambaye ataendelea na ujenzi baada ya mkandaras wa kwanza kushindwa kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa NEC Itikadi, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Amos Makala wakati akizungumza na wakazi wa Buchosa na Bukokwa akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Kauli ya Makala inafuatia baadhi ya wananchi wa Mji wa Bukokwa kumuuliza ni lini barabara hiyo itakamilika, kwani imekuwa ni kilio cha mara kwa mara kupata barabara ya lami.
Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan aliidhinisha fedha na kutolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa barabara.

Makalla amewataka wananchi wa Jimbo la Buchosa kutokumhukumu Mbunge wa Jimbo hilo dhidi ya barabara hiyo kwa kuwa Serikali ilikwishachukua hatua kwa mkandarasi wa awali kwa kususua katika utekelezaji wa mradi huo.