The House of Favourite Newspapers

Makalla amtaka mkandarasi kuikabidhi MV Mwanza Agosti

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  CPA Amos Makalla ameitaka Kampuni ya Gas Entec ya Korea Kusini kukamilisha Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza (Hapa kazi Tu) ifikapo Agost 29, 2023 kwa mujibu wa Mkataba. Ametoa agizo hilo mapema leo Julai 10, 2023 kwenye kikao kazi kilichofanyika Ofisini kwake kilichowakutanisha Kampuni ya Huduma za Meli na Mkandarasi wa mradi huo huku kikiangazia Maendeleo ya Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza inayojengwa kwa zaidi ya Shilingi Bilioni 109 za kitanzania .

“Kwa mujibu wa Mkataba tunapaswa kupokea Meli hii ifikapo tarehe 29 Agosti mwaka huu, na tumeshalipa fedha kwa asilimia 88 na kwa kazi zilizofanyika lakini hadi sasa imefikia asilimia 85 na nilitaka kujua nini kimechelewesha kazi hiyo ambapo nimeambiwa chanzo ni Malighafi kuchelewa kutoka nje,” amesisitiza. Aidha amesema Serikali haina mpango wa  kuongeza muda kwa Mkandarasi anayejenga Meli hiyo ambayo kwa miaka minne imekua ikijengwa na ana imani kikao kazi hicho kitasukuma ukamilishaji kwani siku za karibuni Mhe. Rais amekagua ujenzi na anatarajia kuja mwenyewe kwenye Uzinduzi.

“Tumekubaliana wafanye kazi usiku na mchana ili kufikia Agosti 29, 2023 wawe wamekamilisha Ujenzi huo na waongeze wataalamu ili kusiwe na sababu zingine za kuchelewesha na nimewaagiza waje na mpango kazi mpya ambao ukamilishaji wa ufanisi utaendana na tarehe ya mkataba.” CPA Makalla.