The House of Favourite Newspapers

MAKAMBA, SIRRO WAONGOZA KUAGWA MKE WA KANGI LUGOLA

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro (kushoto) na Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Palamagamba Kabudi,  wakiwa na viongozi wengine kwenye msiba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Group, Eric Shigongo,  akimpa pole mfiwa, Kangi Lugola.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,  Muungano na Mazingira, January Makamba, akisoma salamu za rambirambi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Kangi  Lugola akizungumza jambo kwa niaba ya familia kuhusiana na kifo cha mke wake, Mary Lugola.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, akitoa pole kwa niaba ya bunge.
 Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole,  akitoa salamu za pole kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya wafiwa wakiwa katika huzuni.
Ofisa wa polisi akitoa salamu za pole kwa niaba ya jeshi la polisi.
Shigongo (wa tatu kulia) akitoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Waombolezaji wakipita mbele ya jeneza la Mary Lugola.
Spika Mstaafu, Anne Makinda (katikati) akiwa na aliyekuwa waziri,  George Simbachawene (kushoto na Naibu Spika, Dkt. Ackson.
Kangi Lugola akiwa na baadhi ya wanafamilia wake.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (katikati) akiwa ameungana na waombolezaji.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba,  na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro,  leo wameongoza mamia ya waombolezaji katika kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mary Lugola, ambaye pia ni mke wa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Kangi  Lugola nyumbani kwao, Gerezani Railway Club jijini Dar.

 

Akitoa heshima zake za mwisho kwa niaba ya familia, mume wa marehemu, Kangi Lugola, ameeleza alivyoishi na  marehemu na ujumbe wa mwisho aliomtumia wa kumtakia heri ya Mwaka Mpya saa chache kabla ya kuaga dunia.

 

“Nikiwa katika majukumu yangu ya kikazi nje ya Dar, nilikuwa nikiwasiliana na mke wangu kwa ukaribu sana. Hata katika kujaza zile fomu za Sekretarieti ya Maadili alinipigia simu nikajaza naye kwa zaidi ya lisaa hadi nikahisi sikio linauma.

 

“Ilipofika siku ya mkesha wa mwaka mpya Desemba 31, mwaka jana, mke wangu alinitumia ujumbe mimi  na familia yangu kwa kuwa tuna kundi la familia la WhatsApp, akatutakia heri ya Mwaka Mpya na kuniambia ataongea na daktari aweze kumpa ruhusa kwa kuwa anajisikia vizuri hivyo asherehekee na sisi sikukuu hii. Mwisho wa yote ikashindikana akawa ametangulia mbele za haki, inaniuma sana. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina,” alisema Lugola.

 

Katika tukio hilo la kuuaga mwili wa Mary Lugola, viongozi mbalimbali wa serikali na vyama walihudhuria wakiwemo, Spika Mstaafu, Anne Makinda, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na wengineo kutoka jeshi la polisi.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Group, Eric Shigongo na wengineo.

Marehemu Mary Lugola pia alikuwa Ofisa Mnadhimu Kikosi cha Polisi Reli Tanzania hadi umauti unamkuta.

Comments are closed.