The House of Favourite Newspapers

Makambo, Tambwe Watenganishwa Yanga

MASTRAIKA wawili wa kigeni wa Yanga, Amissi Tambwe na Heritier Makambo hawataanza kwa pamoja kwenye kikosi cha kwanza, Kocha Mwinyi Zahera amethibitisha.

 

Tambwe ni moja kati ya washambuliaji wazuri kwa upachikaji mabao ingawa msimu uliopita alishindwa kutamba kutokana na kuwa nje karibu msimu mzima na kushindwa kucheza.

 

Makambo amesajiliwa hivi karibuni na ataanza kuonekana kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mawenzi mjini Morogoro.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Zahera alisema; “Kombinesheni ya Makambo na Tambwe kwa sasa ni ngumu siwezi kuwachezesha kwa pamoja sababu kila mmoja ana vitu vyake vya tofauti hivyo ninahitaji muda zaidi kuweza kuwatengeneza na wakawa kitu kimoja.”

 

“Kwa mfano Makambo ni mchezaji yule anayepambana na kuzunguka kila eneo tofauti na Tambwe yeye anakaa eneo ambalo ni lake na ndiyo inakuwa rahisi kwa kufunga lakini mimi nataka kutengeneza kitu ambacho kinakuwa na manufaa kwao ambacho kitaibeba timu,”alisema Zahera ambaye bado kwenye dirisha dogo la Desemba atasajili.

 

“Ndiyo maana tumepata nafasi ya kujiandaa kipindi hiki ili kuweka mambo kama haya sawa ingawa tunahitaji muda zaidi,” alisema Zahera ambaye anaamini kwamba kikosi alichonacho kinaweza kushindana kwenye ligi ya ndani kwa muda uliopo.

 

Kocha huyo alikuwa na mapendekezo mengi ya wachezaji wa kigeni lakini akakiri kwamba mara kadhaa yalishindikana sababu kubwa ikiwa ni uchumi kudorora ndani ya klabu.

Comments are closed.