The House of Favourite Newspapers

Makamishna ZEC wapinga kurudiwa uchaguzi Zanzibar

0

1
Makamishna wa ZEC wakipinga kurudiwa uchaguzi wa Zanzibar wakati wakiongea na wanahabari leo jijini Dar.

Wakati wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa wakipinga kile kinachoendelea visiwani Zanzibar, nao makamishna wawili wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Ndugu NASSOR KHAMIS MOHAMED na AYOUB HAMAD wameibuika jijini Dar es salaam leo na kupinga marudio ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu kwa madai kuwa uchaguzi huo sio halali kulingana na matukio yaliyotokea tangu kufanyika kwa uchaguzi halali wa Oktoba 25 mwaka jana.

Wakizungumza na wanahabari Jijini Dar es salaam makamishna hao wamesema kuwa sababu kubwa ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo ni kutokana na kuvurugwa kwa katiba ya Zanzibar tangu tukio la kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana ambapo wamesema kuwa mwenyekiti wa Tume hiyo hakuwa na mamlaka ya kisheria kufuta uchaguzi huo bila kuwashirikisha makamishna wa tume hiyo.

2

Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar NASSOR KHAMIS MOHAMED akizngumza na wanahabari (hawapo pichani) mapema leo jijini Dar es Salaam.

Wamesema kuwa sababu nyingine inayowafanya kupinga uchaguzi wa marudio ni kutokana na kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka jana ambapo uchaguzi huo ulikuwa umekamilika na baadhi ya washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani walishakabidhiwa vyeti vyao na mawakala kusaini kuwa uchaguzi huo hauna kasoro hivyo wanashangaa kuambiwa kuwa uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi zilizopelekea kuubatilisha uchaguzi huo.

Wameongeza kurudiwa kwa uchaguzi huo ambao unatarajiwa kutumia zaidi ya bilioni saba hadi kukamilika kwake ni matumizi mabaya ya rasilimali za taifa kwani uchaguzi Zanzibar ulishafanyika na tayari na kinachoendelea ni mbinu za kuubatilisha uchaguzi huo.

Wameongeza kuwa tukio la kufutwa kwa uchaguzi huo lilitanguliwa na matukio kadhaa ambayo yalionyesha wazi kuwa kuna kikundi cha watu ambacho kinamshauri mwenyekiti wa tume hiyo JECHA SALUM JECHA na sio maamuzi ya tume nzima.

3

Mjumbe mwingine AYOUB HAMAD akifafanua jambo mbele ya wanahabari (hawapo pichani) kuhusu kile kinachoendelea Zanzibar.

“Tarehe 26 oktoba mwaka jana CCM walileta barua ya malalamiko na kumtaka mwenyekiti na tume kufuta uchaguzi huo wakati tayari tulishaanza kutoa vyeti kwa washindi, ambapo mwenyekiti aliitisha kikao cha tume na tulipitisha kwa pamoja kuwa maombi ya CCM hayakuwa na mashiko hivyo mchakato unaendelea” amesema NASSOR KHAMIS ambaye ni mmoja wa makishna wa tume hiyo.

Ameendelea kusema kuwa baada ya maamuzi ya tume ndipo siku iliyofuata mwenyekiti JECHA hakufika katika ujumuishaji wa matokeo kwa siku nzima na ndipo waliposikia kuwa ametangaza kufuta uchaguzi bila kuwashirikisha wajumbe wengine wa tume hiyo na baada ya hapo ndipo ofisi yetu ilianza kuzungukwa na wanajeshi na kuamuriwa tusifanye lolote huku jaji mkuu wa mahakama ya Zanzibar naye akiwa amekamatwa na kupekwa polisi.

Wamesema kuwa kwa matukio kama hayo wanaamini kuwa tume hiyo imeacha kufanya kazi zake kisheria na sasa inafanya kazi kisiasa jambo ambalo linampotezea sifa mwenyekiti wa ZEC kuendelea kuiongoza tume hiyo.

Aidha wamesema kuwa hali iliyopo ndani ya tume kwa sasa sio hali ya kawaidia ambayo inaweza kusimamia uchaguzi wa haki kwani wajumbe wamekuwa wakipingana kwa kila hoja inayoletwa jambo ambalo linafanya uchaguzi wa marudio kutiliwa mashaka na wajumbe wengi wa tume hiyo.
Wajumbe hao wa ZEC wametoa wito kwa wajumbe wengine ndani ya tume hiyo kuacha kufuata mkumbo na kuamua kusimamia sheria inavyosema ili kuwapatia wazanzibar haki yao ya kikatiba

CHANZO: Habari24 Blog

Leave A Reply