The House of Favourite Newspapers

Makamu mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi amjibu Mbatia

0

Kamishna wa NCCR-Mageuzi wa Mkoa wa Ruvuma, Mchatta Eric Mchatta (kushoto) akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, Leticia Ghatti Mosore, na mwakilishi wa NCCR-Mageuzi, Hamlyn Erasto.

Leticia Mosore (katikati) akisoma taarifa yake.

Wanahabari wakichukua matukio katika hafla hiyo.

Mkutano ukiendelea.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Tanzania Bara, Leticia Ghatti Mosore, aliyesimamishwa na Mwenyekiti wake James Mbatia amesema hakuridhishwa na utaratibu uliotumika kumwajibisha.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar, Mosore amesema kuwa Mbatia amemfukuza bila kufuata Katiba ya Chama ambayo kupitia ibara ya 27 (3) kifungu (C) inasema kuwa makamu mwenyekiti ataweza kuondolewa kwa mapendekezo ya halmashauri kuu ya taifa ya chama hicho kwa kura zaidi ya nusu za wajumbe halali.

Amefafamua kuwa Mbatia katika utetezi wake alidai kufuata kanuni hiyo kupitia kikao cha maadili walichokaa Septemba 22 mwaka huu ambacho alisema hakikuwa halali kwa kuwa kiliundwa na watu wachache wenye uhusiano wa kifamilia na undugu na Mbatia.

“Hata kama kikao hicho kingekuwa kikao halali bado kingekiuka haki ya msingi ya binadamu ya kupewa muda wa kujitetea, isitoshe kanuni za chama zinafafanua vizuri kwamba lazima mtuhumiwa apewe majuma mawili ya kujitetea kimaandishi ambayo mimi makamu mwenyekiti sikupewa,”alisema Leticia.

Aidha amesema kuwa taarifa za kufukuzwa kwake alizipata kupitia magazetini Oktoba Mosi mwaka huu ambapo sababu kuu za kufukuzwa kwake zilitajwa kuwa anatumika kukihujumu chama kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupanga njama za kumdhuru mwenyekiti wake.

Leticia amekanusha madai hayo na kumtaka Mbatia athibitishe kwa kuwataja viongozi wa CCM anaoshirikiana na akazidi kusimamia kauli yake aliyoitoa kabla ya kusimamishwa kwamba haridhishwi na mwenendo wa ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa NCCR-Mageuzi kupewa majimbo 12 tu ambapo sita tayari yamekwishaingiliwa na CHADEMA hivyo uwezekano wa kushinda kwenye majimbo hayo ni mdogo kwa kuwa kura zitagawanyika.

(NA DENIS MTIMA/GPL)

Leave A Reply