The House of Favourite Newspapers

Makamu Wa Rais Dkt. Mpango; Waelimisheni Wananchi Umuhimu Wa Usuluhishi

0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini leo tarehe 22 Januari, 2023 katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa rai kwa Mahakama na Wadau wake kuelimisha wananchi kuhusu njia bora zaidi ya utatuzi wa migogoro yao na hususani njia ya usuluhishi ambayo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda.

Akizungumza mapema leo tarehe 22 Januari, 2023, katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo amesema kuwa, kuna umuhimu wa kuwa na mfumo thabiti wa kutatua migogoro ili kuokoa muda unaotumika katika uendeshaji wa kesi kwa njia ya kawaida.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kwa ajili ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria kwa mwaka 2023.

Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni; Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.

“Napenda nikiri wazi kwamba, nimefurahishwa na Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu ambayo inahimiza Usuluhishi kama njia mojawapo ya utatuzi wa migogoro ambayo kimsingi una faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, kupunguza mlundikano wa mashauri, kukuza uchumi wa Taifa na nyingine,” amesema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa nne kushoto), Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji na Viongozi wengine walioketi meza kuu wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuanza kwa shughuli ya ufunguzi wa wiki ya Sheria, 2023.

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango amewaomba pia Viongozi wa dini kuwakumbusha waumini wao kuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi huku akiwahamasisha wananchi kutembelea mabanda ya Mahakama na wadau katika Maonesho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria yanayoendelea nchi nzima.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Mpango amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuuongoza vyema Mhimili wa           Mahakama hususani katika kusimamia uboreshaji wa huduma ikiwemo matumizi ya TEHAMA mahakamani, uboreshaji wa usimamizi wa mashauri, miundominu ya majengo ya Mahakama na kadhalika.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (katikati) wakati Kiongozi huo alipotembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Utoaji elimu ya sheria

“Naipongeza Mahakama ya Tanzania hususani Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma kwa kuendelea kuiongoza vyema Mahakama katika kuboresha huduma zake, kwa kifupi naweza kusema ‘you have transformed Judiciary to the next level’” amesisitiza Makamu wa Rais.

Kadhalika, Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba kuihusisha Mahakama ya Tanzania kikamilifu katika Dira ijayo ya Taifa ambayo ipo kwenye mchakato wa kuandaliwa .

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kuhusu Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi kutoka kwa Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Wanjah Hamza (kulia). Wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kushoto kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani.

 

Hata hivyo, Mhe. Dkt. Mpango amewakumbusha Viongozi wa Mahakama kuendelea kufanyia kazi changamoto kadhaa za Mahakama ambazo ni pamoja na kuwawajibisha baadhi ya watumishi wa Mhimili huo ambao wanajihusisha na vitendo cha rushwa na ukiukwaji mwingine wa maadili na nyingine.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa, wananchi walio wengi bado hawafahamu taratibu hizo na pia kuelewa ni namna gani sheria na taratibu zake zina uhusiano na uchumi au zinavyoweza kuathiri shughuli zao za kila siku za kijamii, kiuchumi, na uzalishaji mali.

Mahakama inafahamu kwamba sio wananchi wote tunaowahudumia wanafahamu vema haki na wajibu wao katika taratibu za kupata haki zao pale ambapo migogoro itaibuka. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa utoaji haki kila mwaka hutumia maadhimisho ya wiki ya sheria kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kufahamu taratibu mbalimbali za kupata haki na pia kuwaelimisha juu ya haki na wajibu wao katika kupata haki,” amesema Mhe. Prof. Juma.

Sehemu ya Majaji wastaafu, Majaji waliopo kazi na wageni waalikwa wengine wakifuatilia kwa makini hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria

 

Akizungumzia suala la Usuluhishi, Mhe. Prof. Juma amesema wananchi wana wajibu wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi huku akitoa wito kwa wananchi kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria na hususani Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi ili kupata elimu na uelewa zaidi kuhusu njia hiyo iliyosheheni faida lukuki kwa kufanya hivyo kutawapa nafasi ya kufanya shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Taifa.

Ni muhimu wananchi wafahamu pia namna ambavyo migogoro ya biashara, kazi au mikataba inayoweza kutokea kwa njia za mitandao; na inavyoweza kutatuliwa (ikiwemo kwa njia ya usuluhishi) kwa njia ya TEHAMASilaha bora ya kupigania Haki ni kuelewa upatikanaji wa hiyo Haki unayopigania ipo chini ya Sheria, Kanuni au Taratibu zipi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Ameongeza kwamba, utoaji elimu unatarajiwa kutolewa kwa namna mbalimbali ikiwemo vipindi vya redio, midahalo, na maonesho katika maeneo mbalimbali nchi nzima kwa kipindi chote cha maadhimisho lengo ni kuwafikia wananchi wengi hata wale wa vijijini kadri inavyowezekana. Huku akitoa wito kwa wananchi kutumia fursa hii muhimu kwao kufuatilia elimu itakayotolewa.

Maonesho haya yaliyozinduliwa leo yatafanyika kwa muda wa siku nane ambapo yanatarajiwa kukamilika tarehe 29 Januari, 2023 ambapo yatahitimishwa kwa kilele cha Siku ya Sheria itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2023 huku mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Leave A Reply