Makocha Simba, Yanga Wachimbana Mkwara -Video

KATIKA kuhakikisha kila upande unafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, makocha wa timu za Simba na Yanga, Seleman Matola na Cedric Kaze wametambiana kuhakikisha wanaibuka na pointi tatu katika mchezo huo wa hitimisho wa michuano hiyo ili kuweza kulitwaa kombe hilo.

 

Simba na Yanga zinatarajia kukutana leo jioni katika Uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar, baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ambapo Simba ilitinga hatua hiyo baada ya kuitoa Namungo FC mabao 2-1 huku Yanga ilitinga hatua hiyo kwa kuitoa Azam kwa penalti 5-4.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti makocha wa timu hizo mbili kuelekea mchezo wa fainali kila mmoja alisema kikosi chake kipo vizuri hawana majeruhi na wanachosubiria ni mechi tu.

 

“Kikosi changu kipo vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Yanga wachezaji wote wapo vizuri tumekiandaa vyema hakuna majeruhi hata kidogo na jioni tutafanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo kila mchezaji anaonyesha morali ya hali ya juu kuelekea mechi hiyo kwani lengo letu ni kuona tunafanikiwa kuibuka mabingwa,” alisema Matola.

 

Aidha kwa upande wa Kaze kupitia Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa:

 

“Kocha amekiandaa vyema kikosi chake amesema anajipanga kuhakikisha anafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, hatuna majeruhi hata mmoja na amekinoa kikosi chake vizuri.“

 

Tumefanya mazoezi asubuhi saa 4 (jana), katika Uwanja wa Amaan tuna kikosi cha wachezaji 18 na jioni tunawapisha wapinzani wetu Simba waweze kufanya mazoezi, Simba ni timu ya kawaida hivyo tunaimani tutafanya vizuri na kuibuka na ushindi katika mchezo huu.

Toa comment