The House of Favourite Newspapers

Makonda Akagua Ujenzi Barabara ya Njia 8, Morocco – Mwenge

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo Jumatatu, Novemba 4, 2019 ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara nne mpya kutoka Morocco hadi Mwenge, Dar.

 

Kukamilika kwa njia hizo kutafanya idadi ya barabara kufikia nane, jambo linalotarajiwa kupunguza na ikiwezekana kumaliza tatizo la foleni kwenye Barabara ya Bagamoyo.

 

Makonda amesema barabara hiyo ina urefu wa KM 4.3 na itagharimu shilingi bilioni 79 hadi kukamilika ikihusisha uwekaji wa taa za barabarani, vivuko, mitaro, sehemu ya kufanyia mazoezi na eneo la watembea kwa miguu.

 

Ujenzi huo unaenda sambamba ujenzi wa mferegi mkubwa na wa kisasa wa kusafirisha maji ya mvua kutoka Shekilango, maeneo yote ya Sinza, Mwenge, Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama kupitia Mikocheni eneo la Tanesco na kuyapeleka hadi baharini, jambo litakalosaidia kumaliza kero ya maji kipindi cha mvua.

Makonda amesema katikati ya barabara hiyo kumeachwa kwa ajili ya Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi huku akimshukuru Rais Dk John Magufuli kwa namna anavyozipatia majibu kero za wakazi wa Dar.

 

Pamoja na hayo, Makonda amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa service road yenye upana wa mita 6.5 kuingilia stendi mpya ya Mwenge kutokea Bamaga pamoja na kuunganisha barabara za Sinza-Mapambano, barabara ya nyuma ya Chuo cha Ustawi wa Jamii kutokea Barabara ya Akachube.

 

Hata hivyo, Makonda amesema upanuzi wa barabara ya njia nne kutoka Shekilango hadi Bamaga unatarajiwa kuanza siku yoyote kuanzia sasa kwa kuwa fedha zipo.

 

Katika ziara hiyo, Makonda ametembelea pia Mradi wa Ujenzi wa Barabara na Mitaro ya maji ya mvua eneo la Bwawani Kata ya Mwananyamala ambalo kwa muda mrefu wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakiteseka na kero ya maji kujaa na kutuwama katika makazi yao, lakini sasa wanafurahia barabara nzuri na mitaro ya kisasa ya kupitisha maji.

Na Neema Adrian

 

Comments are closed.