MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema licha ya wabunge kuwatumia vijana kujipatia kura, wamekuwa nyuma katika kuhudhuria shughuli za msingi za maendeleo ambapo aliwataja wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Halima Mdee (Kawe) na John Mnyika wa (Kibamba).
Makonda aliyasema hayo leo Novemba 27, 2018, katika hafla ya ufunguzi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uliofanywa na Rais John Magufuli.
Maktaba hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja na kuhifadhi vitabu 800,000.
“Hata yule mbunge wa Ubungo (Saed Kubenea- Chadema) ambaye chuo hiki kipo katika jimbo lake sijamuona, kwa kweli nampongeza sana (waziri mkuu wa zamani) Edward Lowasa kwa sababu anaoneka kukubali juhudi zako unazozifanya,” alisema Makonda akimsifia Rais Magufuli na kuongeza:
“Kwa masuala ya elimu mkoa wetu umekuwa wa kwanza kwa upande wa shule za msingi kwa ufaulu wa asilimia 92, kidato cha sita pia wamefanya vizuri sana ambapo tumepata ufaulu wa asilimia 97.”
Maktaba hiyo mpya, inaongoza kwa ukubwa Afrika Mashariki na Kusini ikiwa imeunganishwa na umeme wa jua kwa kiwango cha kilovolt 280 zenye uwezo wa kuwasha taa na viyoyozi ambapo imegharibu Dola 41,280 milioni za Marekani huku chuo kikitoa Sh1.78 bilioni kwa ajili ya kugharamia nakala za vitabu na majarida.
Pia, ina ukubwa wa kilomita za mraba 4.4 ikiwa na kompyuta 160 zinazowezesha wanafunzi kusoma vitabu kwa njia ya mtandao.
Comments are closed.