The House of Favourite Newspapers

Makonda Aongeza Nguvu Tamasha Kubwa la Vijana Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amejitokeza kuongeza nguvu kwenye tamasha la wanachuo na vijana kutoka pande mbalimbali za Jiji la Dar, linalotarajiwa kufanyika Novemba 15, mwaka huu.

 

Tamasha hilo kubwa la kiroho linaloendana na burudani ya muziki linaandaliwa na Kanisa la Kanisa la TAG–Victory Christian Centre Tabernacle kwa kushirikiana na Jumuiya za Kikristo na Serikali za wanafunzi wa vyuo kabla ya kuongezewa nguvu na Makonda.

 

Akizungumza na wanahabari kwenye kanisa hilo lililopo Kawe Beach jijini Dar Alhamisi iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Mchungaji Dkt Huruma Nkone amesema linatarajiwa kufanyika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar.

 

Mchungaji Nkone amesema tamasha hilo ambalo limekuwa likitumika kuwapa moyo na kuwajenga kiroho vijana hao, limeshafanyika mara nane kwa mafanikio makubwa.

 

Dkt. Nkone ambaye atakuwa mhamasishaji wa kuwajenga kiroho na kiakili vijana hao, amewataja wazungumzaji wengine kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo, Samuel Sasali, Dkt. Hellen Gwambaye na Salome Msimbe.

 

Dkt. Nkone amesema amehakikishiwa na Makonda uwepo wa usalama wa kutosha kwa watakaohudhuria tamasha hilo wao pamoja na mali zao.

 

Tamasha hilo pamoja na kuwajenga kiuzalendo vijana hao, litapambwa na burudani kutoka makundi mbalimbali ikiwemo Zabron Singers, Upendo Nkone, Joel Lwaga, Walter Chilambo, Students Mass Choir, Beda Smith, Hype Squad Dancers na Rivers of Joy International.

 

Kwa upande wake Shigongo alisema tamasha hilo lina msingi mkubwa sana wa kuwajenga kiroho vijana hao na kusema usipowajenga vyema vijana si rahisi kupata taifa bora.

 

“Vijana wanatakiwa kupewa hamasa na kujengwa kiroho ili waweze kufikia malengo yao.

“Tukiwa na taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu, ni lazima tupige hatua kubwa ya kimaendeleo.

 

“Tatizo kubwa lililopo hapa nchini kwa sasa ni vitu kama kukosa uaminifu, hivyo kutoaminiwa jambo ambalo linawafelisha wengine kwenye koneksheni za mafanikio,” alisema Shigongo na kuwataka vijana kufika kwa wingi kwenye tamasha hilo ambalo kiingilio ni bure.

 

RICHARD BUKOS, Dar es Salaam.

SHUHUDIA WAKISAKATA RUMBA

 

Comments are closed.