The House of Favourite Newspapers

MAKONDA AWAOMBA MSAMAHA WACHAGGA, ASKOFU AMPATANISHA NA MBOWE – VIDEO

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Bashiru,  amemwombea msamaha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kauli yake kwamba ni ajabu kwa watu wa kabila la Wachagga kutoa fedha kusaidia walemavu.

 

Makonda alisema maneno hayo wakati wa kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam wanzoni mwa wiki hii.

 

“Baba Askofu hatujafanya kazi ya kuwaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora, sasa tunavuna matunda yake, naomba nimuombee msamaha kijana wangu Makonda, nilimsema Simiyu mara ya kwanza, akaja ofisini analia, ameanza kujirekebisha,” alisema  Bashiru wakati wa ibada ya kumwombea marehemu Mengi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Moshi Mjini.

Awali, akitoa risala ya rambirambi, Mwenyekiti wa Chama cha Demorasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja na mambo mengine,  aliwataka Watanzania kutogombanishwa na kauli za viongozi hasa za kikabila na kidini huku akiwataka viongozi kutafakari maneno kabla ya kuyaongea kwani yangeweza kuwagawa watu na kuleta machafuko.

 

“Tuna nchi moja ambayo tunastahili kupendana na kusaidiana, na kila mtu ana haki ya kumsaidia mwenzie, tusikubali kauli za viongozi zitugawe na hasa za kidini na kikabila, kauli ya kusema kuna makabila hayawezi kuwasaidia walemavu si nzuri na haikutupendeza kwa kweli, tujitafakari tunapotaka kuongea maneno,” alisema Mbowe.

 

Baada ya hotuba hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo, aliwaita  Makonda na  Mbowe akisema hiyo ni ishara ya kusameheana na kufikia mariadhiano na akawataka wapeane mikono ambapo baadaye Makonda alisema hakuwa na nia mbaya ktika kauli yake ila tafsiri “ilileta shida” hivyo akaomba msamaha na kuendelea:

“Namshukuru Katibu Mkuu kwa kuomba radhi kwa niaba yangu, hakika ni upendo wa hali ya juu. Ninahisi tafsiri inaweza kuwa ni tatizo na mimi niombe radhi kwa tafsiri hiyo kwa sababu nimemsifia Mchagga katikati ya Wachagga, sio Mchagga tofauti na kabila jingine. Napokea na nitaendelea kumuenzi Mzee Mengi kwa mema yote aliyoyafanya hasa kwa mkoa wetu kuwahudumia walemavu kwa sababu amekuwa alama ambayo daima haitafutika.”

Katika ibada hiyo Askofu  Shoo alisema: “Dhambi nyingine tunayotakiwa kuitubu ni ya wenye nafasi kuwakanyaga walio wadogo, leo mtu anapata vimilioni kadhaa anataka atembee juu watu, unapata kacheo sijui U-DC, U-RC, Uwaziri, unawaona wenzako si kitu; acha kiburi.

 

“Mungu atusaidie tusibaguane kwa misingi yoyote ile, dhambi ya kubaguana tunapaswa kuitubu, tuache. Tuache kiburi hasa viongozi wa huu umri mdogomdogo, mnajitutumua kama chatu, kifutu, Bwana atawashusha, usitumie nafasi yako kunyanyasa wengine.”

MAKONDA AMUOMBA MBOWE MSAMAHA, ASKOFU AWAPATANISHA!

Comments are closed.