The House of Favourite Newspapers

MAKONDA AYAKANA MAKONTENA 20 YALIYOSHIKILIWA BANDARINI

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema hajui chochote kile kuhusu kudaiwa au makontena 20 yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika Bandari Kuu ya Dar es Salaam .

 

Hivi karibuni TRA, ilitangaza kusudio la kupiga mnada makontena 20 za Paul Makonda ikiwa atashindwa kuyalipia ushuru na kuyachukua ndani ya siku 30 kuanzia Jumatatu. Makontena hayo ambayo yanasadikiwa kuwa ndani yake yana samani za ndani na ofisi, yamesubiri utaratibu wa kuyatoa TRA kwa zaidi ya siku 90 zinazokubalika kwa mujibu wa sheria za kodi.

 

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kuwa kwa kawaida bidhaa zote zinapoagizwa na kufika bandarini zinatakiwa kuondolewa ndani ya siku 90. Kayombo alisema inapotokea muda huo ukapita bila wahusika kuondoa mizigo yao, hujulishwa na mamlaka hiyo kwa kupewa notisi ya siku 30 ili waondoe.

 

Kwa mujibu wa tangazo la TRA lililotoka kwenye vyombo vya habari Jumatatu, Mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa wateja nane akiwamo “Paul Makonda” ambao mizigo yao imekaa bandarini zaidi ya muda unaotakiwa.

 

Katika tangazo hilo, Kamishna wa Idara ya Kodi ya Ushuru wa Forodha na Bidhaa, ametoa siku 30 kwa wamiliki wa mali mbalimbali zilizopo katika ghala la TRA kwenda kuzichukua la sivyo baada ya muda huo zitapigwa mnada kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa ushuru wa forodha.

 

Kayombo alisema kuwa, mzigo unapopitiliza muda wa kukaa bandarini, TRA huwakumbusha wahusika kwa kuwapa notisi kama ya siku hiyo.

Comments are closed.