The House of Favourite Newspapers

Makonda; Hata Kama ni Vigogo; Wataje Umma Upo Nyuma Yako

MAKALA: NA ELVAN STAMBULI | UWAZI | NIONAVYO MIMI

WIKI iliyopita tulimsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akisema ameanzisha vita dhidi ya madawa ya kulevya katika mkoa wake, akawataja wasanii na polisi kadhaa akiwatuhumu kuhusika kwa njia moja au nyingine na biashara hiyo. Tumuunge mkono.

Nashauri vita hii iwe  kwa mikoa yote, yaani iwe ni vita ya nchi nzima. Nionavyo mimi ni kwamba tatizo la madawa ya kulevya nchini limeendelea kukua licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kupambana nalo.

Paul Makonda akiwa amezungukwa na vijana wanaosemekana kutumia dawa za kulevya.

Hali hii inadhihirishwa na kiasi kikubwa cha madawa ya kulevya kilichokamatwa hususan heroin na cocaine, kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi aliwahi kusema kuwa  katika mwaka 2011madawa hayo yaliingizwa mengi ikilinganishwa na mwaka 2012.

Alisema takwimu zilionyesha kuwa kilo 264.3 za heroin zilikamatwa mwaka 2011 ikilinganishwa na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka 2010. Takwimu hizi zinaonyesha ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu.

Paul Makonda akizungumza jambo mna kijana mdogo mahabusu.

Aidha, mwaka 2011 kilo 126 za cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa mwaka 2010 ambalo ni ongezeko la asilimi 100. Ongezeko hili la ukamataji linaashiria kukua kwa biashara hiyo haramu ya madawa za kulevya kunalorahisisha upatikanaji wa madawa hayo na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya watumiaji nchini.

Biashara haramu ya madawa ya kulevya inachochewa na mambo mbalimbali yakiwemo mmomonyoko wa maadili katika jamii, tatizo sugu la rushwa, uchu wa kutaka utajiri wa haraka, uelewa mdogo wa athari za madawa ya kulevya na ukosefu wa ajira.

Aidha, kuwepo kwa mfumo dhaifu wa udhibiti husababisha kushamiri kwa biashara na matumizi haramu ya madawa ya kulevya nchini. Matumizi hayo huathiri afya za watumiaji, kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa na kuongeza umaskini. Vilevile, biashara hiyo haramu huchochea uhalifu wa aina mbalimbali ukiwemo wizi, ujambazi, ubakaji na rushwa.

Tuliambiwa kuwa katika kipindi cha mwaka 2011, serikali iliendelea na jitihada za kupambana na biashara na matumizi haramu ya madawa ya kulevya. Jitihada hizo ni pamoja na kukamilisha Rasimu ya Sera ya Taifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya, kuanzisha mchakato wa kuwa na chombo madhubuti cha kupambana na madawa ya kulevya. Vilevile, Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Madawa ya Kulevya (Sura 95) ilipitishwa ili kuongeza adhabu kwa wafanyabiashara wa madawa hayo.

Nionavyo mimi ni kwamba nyuma ya watumiaji wa madawa haya, kuna kundi la wanaoyaleta madawa hayo ambayo thamani yake hutajwa kuwa ni kubwa. Wapo waagizaji ambao hutajwa kuwa ni mapapa na wasambazaji. Ni akina nani hao?

Hawa ndiyo tatizo kubwa, ndiyo wanaowalipia watu nauli kwenda kuleta ‘mzigo’ huko nje kwa sababu hatuna viwanda vya madawa haya nchini.

Watu hawa wapo katika jamii yetu tunaishi nao na ndiyo maana nasema Makonda inafaa aungwe mkono na umma wote wa Watanzania ili hao wote wasambaratishwe.

Wenye biashara hii hawajali ustawi wa vijana wetu, fikiria, kijana anakuwa zezeta, wao wanajali kupata fedha na kujitajirisha tu. Kwa asilimia kubwa wanaoleta madawa hayo nchini watoto wao hawayavuti, hivyo wapo radhi kuwafanya vichaa watoto wa wenzao! Hawana uzalendo hawa na wanalitia taifa hasara kubwa kwani mwaka 2011 serikali iliendelea kutoa tiba na kuwezesha huduma za kusaidiana miongoni mwa watumiaji (Self help ground/sober houses), kuendelea na matayarisho ya utoaji tiba ya methadone.

Nampongeza Makonda  na  vyombo vya dola hasa watendaji waliofanikisha kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha madawa ya kulevya aina ya heroin na cocaine, lakini bado kuna shida wanapofikishwa mahakamani.

Tuliwahi kushuhudia watuhumiwa kutoka nje ya nchi wakifikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na kilo nyingi za madawa hayo lakini wakaachiwa kwa dhamana! Tulibaki tukijiuliza sheria zinasemaje? Kwa nini waliachiwa? Jibu unalo wewe msomaji!

Ajabu ni kwamba baada ya kuachiwa walipewa hati zao za kusafiria na kukimbilia nje ya nchi. Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Nchini, Godfrey Nzowa kwa vyovyote yeye na vijana wake waliofanya kazi hiyo ya kukamata, walikatishwa tamaa na idara ya mahakama. Tujiulize, huyu anayefanya hivyo mahakamani tumchukuliaje?

Rai yangu kwa wizara mbalimbali, taasisi za serikali, asasi za kiraia, mashirika ya dini na wadau wengine tumuunge mkono Makonda katika mapambano haya dhidi ya madawa ya kulevya.

Nakumbusha kuwa jukumu la kupambana na madawa ya kulevya ni letu sote. Hivyo  tuunganishe nguvu zetu ili kukabiliana na tatizo la biashara na matumizi haramu ya madawa hayo. Ni wajibu wetu tukiwa raia wazalendo kufanikisha azma ya kujenga taifa lisilovumilia biashara na matumizi ya madawa ya kulevya, wanaowajua mapapa, waende kwa Makonda au Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Nijuavyo ni kwamba taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini huandaliwa kila mwaka na tume ya kuratibu udhibiti wa madawa hayo na kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Madawa ya Kulevya (Sura ya 95), sijui kama hilo linafanyika, lakini hii vita ni yetu sote; siyo ya Makonda na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, CP Simon Sirro tu, uzuri hata Rais John Magufuli jana aliunga mkono vita hii.

Ni matarajio yangu kuwa vita hii iliyoanzishwa na Makonda itasaidia kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara haramu ya madawa ya kulevya na kuondoa athari zitokanazo na janga hili lakini nasisitiza, vita isambae nchi nzima kwani hao wajanja wanaweza kufikiria kwenda kufanya uhalifu huo katika mikoa mingine.

Kwa stori zote kali, Tu-follow

Facebook @Globalpublishers

Twitter @GlobalHabari

Instagram @GlobalPublishers

YouTube @GlobalTVTZ

Save

Comments are closed.