The House of Favourite Newspapers

MAKONDA, HUU HAPA UFUSKA WA KUTISHA!

VITUKO katika Jiji la Dar es Salaam sijui vitaisha lini? Maana kila uchwao ya kusikia ni mengi; Ijumaa linakupakulia tukio jipya la ufuska wa kutisha.  

 

Tangu wiki hii ianze, masikio yamekuwa bize na mambo ya video chafu ya mwanadada Ruth Abubakar ‘Amber Rutty’ iliyomuibua Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda na kuanzisha oparesheni takasa jiji akianzia na ishu ya kutokomeza ushoga.

 

Wakati zoezi la Makonda likiendelea kwa watu kumtumia meseji ‘kuwachoma’ wanaofanya mambo machafu, Ijumaa likanasa ishu nyingine nzito inayowahusisha mabinti wadogo kufanya ngono katika nyumba ya mfanyabiashara anayeishi Mikocheni.

 

KAA TAYARI KWA HABARI

Mwishoni mwa wiki iliyopita, chanzo chetu kinachoishi Mikocheni kililitonya gazeti hili kuwa kuna mfanyabiashara eneo hilo amefungua saluni ya kuchua misuli ‘Massage’ inayotoa pia huduma ya ngono. “Kuna wasichana wadogo wapo pale, ukifika kwa ajili ya masaji utafanyiwa, lakini wanaume wengi wanaokwenda pale wanafuata vile vibinti,” chanzo kilidai.

 

POLISI WAJULISHWA

Aidha chanzo hicho kiliongeza kuwa taarifa za kituo hicho cha masaji zimeshafikishwa polisi kwa uchunguzi zaidi. “Nilishawasiliana na polisi, walichoniambia nikiona wanaume wanaowanunua wale wasichana wameingia niwaambie. “Sasa na ninyi muwe tayari wakati wowote, nikishitukia mchezo tu, nawatonya polisi na ninyi mje mchukue tukio zima,” chanzo chetu kilisema.

KINACHOWAUMA WENGI

Kwa mujibu wa chanzo hicho ni kwamba, kinachowasikitisha majirani wengi wa eneo hilo ni kuwaona wasichana hao wadogo wakifanya kazi hiyo ya hatari kwa afya na inayodhalilisha utu wao. “Mimi kama mzazi inaniuma, hawa mabinti ni wadogo, ukiona mibaba inayoingia humo utawahurumia,” chanzo kilidai na kuainisha kuwa dau la kufanya ngono na mabinti waliomo kwenye nyumba hiyo ni kati ya elfu 20 hadi 30.

 

SIKU YA TUKIO

Jumanne wiki hii, saa 4 asubuhi chanzo kililiambia Ijumaa kuwa soko la wasichana hao lilikuwa limechanganya kutokana na kuingia kwa wateja kadhaa.  “Polisi nimeshawaambia, leo mambo safi njooni,” chanzo kiliweka wazi mchongo ambao ulipewa uzito wa juu ya kikosi kazi cha Ijumaa ambacho kilifika eneo la tukio mapema kabla ya polisi.

 

Kikosi kikiwa eneo la tukio kikisubiri wenye mamlaka ya kuvamia nyumba hiyo wafike, kilishuhudia wanaume wawili wakitoka kwenye kituo hicho cha masaji. Hata hivyo haikufahamika kuwa wanaume wale walitoka mle kununua wale wasichana au ni kufanyiwa masaji kama biashara halali ilivyosajiliwa.

 

POLISI WAFIKA

Subira yavuta heri; baada ya kuwepo eneo la tukio kwa zaidi ya dakika 45 bila polisi kutokea na kuonekana kama mchongo utabuma, ghafla polisi waliingia kwa kasi kwenye nyumba hiyo na kuanza kufanya upekuzi. Bila kusubiri, wapigapicha wetu nao walitinga eneo hilo la tukio na kazi ya kukusanya habari ikaanza.

 

Mbali na kukuta wasichana wengine watatu wakiwa mapokezi wakikaribisha wageni, chumba kimoja kilidaiwa kuwa na mteja akifanyiwa masaji. Wakati polisi wakitaka kuingia katika chumba hicho walipishana na mwanaume mmoja akitoka mbio huku akiwa amelowa mafuta mwilini ambaye aliruka ukuta na kutokomea.

 

Ndani ya chumba hicho alichochoropoka mwanaume huyo alikutwa msichana anayekadiriwa kuwa na miaka chini ya 19 akiwa amejikunyata kitandani huku nguo zake zikiwa zimetupwa chini. Mbali na msichana huyo kukutwa katika hali hiyo, kitandani kulikuwepo pia na mipira mitatu ya kiume huku boksi moja likiwa limefumuliwa lakini mpira haukuwemo ndani.

MSICHANA AHOJIWA

Mara baada ya kutiwa mbaroni na wana usalama, msichana huyo alihojiwa ambapo alikiri kuwa na mwanaume chumbani.

POLISI: Unaitwa nani?

SHADYA: Shadya.

POLISI: Una umri gani?

SHADYA : Miaka 19

POLISI: Hii ni saluni ya masaji au danguro?

SHADYA: Kituo cha masaji.

POLISI: Sasa mbona mlikuwa mnafanya ngono?

SHADYA: Yule baba aliniambia tufanye akasema atanipa hela.

MFANYABIASHARA AITWA

Kutokana na kadhia hiyo polisi walilazimika kumuita mwanamke aliyetajwa kuwa ndiye mhusika wa kituo hicho ambapo alipofika alionesha mshangao wa kile kilichotokea. Hata hivyo polisi walilazimika kuondoka na watuhumiwa kwa madai ya kuwapeleka kituoni kwa ajili ya mahojiano na kukifanya kikosi kazi cha Ijumaa kirejee ofisini kwa ajili ya majukumu mengine.

 

MAKONDA ACHARUKA

Kwa wiki nzima Makonda amekuwa mbongo kutokana na uwepo wa matukio ya ufuska mfululizo ambapo ameagiza kupewa taarifa za watuhumiwa ili washughulikiwe kisheria. Uchafu ambao Makonda uliutaja kuwa anataka kudili nao kisawasawa ni pamoja na ushoga, usambazaji wa picha chafu, umiliki wa madanguro, biashara ya ukahaba na vituo vya masaji kugeuzwa kuwa sehemu za kufanyia ngono.

 

Kwa kuzingatia kauli hiyo ya Makonda, Ijumaa limempa tukio hili jipya la laivu juu ya uwepo wa saluni za kuchua misuli jijini Dar zinazojihusisha na matendo machafu ingawa mara nyingi wachunguzi wetu wamekuwa wakifukua na kuyaanika madanguro na saluni hizo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Comments are closed.