The House of Favourite Newspapers

MAKONDA: “KWA HILI SIOMBI MSAMAHA”, ATAJA CHEO ANACHOKIPENDA – VIDEO

MKUU wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda,  amesema hakuna jambo ambalo halipendi kama kusikia Mkristo akilalamika kwamba hakuna ajira, maisha magumu au hakuna kazi.

 

Makonda amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi, Mei 18, 2019 katika Kongamano la Victory Campus Night 2019 lilofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

“Juzi kati hapa nilikumbuka picha yangu ambayo niliipiga mwaka 2003 wakati nikisoma Chuo cha Uvuvi Nyegezi, Mwanza. Nguo nilizovaa haijulikani ni saizi yangu au ya mtu mwingine, hayo ndiyo maisha ya Watanzania wengi walio maskini.  K kilichobadilisha maisha yangu si marafiki wala elimu, bali ni pale nilipotambua kuwa Yesu ndiye mwokozi wangu.

“Nimejengwa kwenye mwamba imara, kila wimbi linalokuja haliwezi kuning’oa, inawezekana wewe ndiye msomi pekee nyumbani kwenu, lakini una nafasi ya kubadili maisha yako. Wapo watu hapa wanasubiri kwenda mbinguni, lakini ukikutana nao hapa wamechoka hawafanani hata na utajiri wa Baba Yetu wa Mbinguni. Tunafanya maombi ya kutaka kwenda mbinguni, tunasahau principles (kanuni) ambazo Mungu ametupa kwa ajili ya kuishi hapa duniani.

“Unakuta mtu anamaliza chuo na GPA ya 5 halafu hana kazi au anaajiriwa halafu hakuna mabadiliko kwenye hiyo ofisi uliyoajiriwa, hicho si kichwa cha Yesu. Unafikiri kumpata mkuu wa mkoa kama mimi ni mchezo? Nimembeba Kristo, nikiingia mkoani nakuwa naye, ananiwezesha kufanya mambo mengi ya tofauti. Cheo ninachokipenda kuliko vyote ni kuwa mwana wa Mungu.

“Na hili siombi msamaha, ni dhambi kwa Mkristo kulalamika hakuna kazi, hali ni ngumu, hakuna ajira, maana yake sisi ndiyo sababu ya kutengeneza ajira, una uwezo wa kutengeneza kazi ambayo haipo ikawepo, unapaswa kutengeneza ajira, utatembea na bahasha kutuma maombi mpaka bahasha inachanika,” amesema Makonda.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa ameahidi kutoa gharama zake kwa ajili ya kuandaa kongamano kama hilo la Victory Campus Night litakalofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

MSIKIE MAKONDA AKIFUNGUKA HAPA

Comments are closed.