The House of Favourite Newspapers

Makonda: Wanaume Wakatwe 40% ya Mishahara Yao Wapewe Wake Zao

0

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema anatarajia kupeleka muswada binafsi bungeni, kutaka itungwe sheria ambayo itamka mwanamume ambaye ni mfanyakazi, kukatwa asilimia 40 kwa ajili ya mke wake ambaye ni mama wa nyumbani.

 

Makonda alisema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika kimkoa kwenye Viwanja vya Leaders wilayani Kinondoni.

 

Makonda alisisitiza kuwa hataki kumwona mwanamke yeyote katika Mkoa wa Dar es Salaam akinyanyasika, ndiyo maana aliamua kuwasaidia wanawake waliotelekezwa na wenza wao na kutoa namba 0682009009 ambayo wanaweza kupiga bure.

 

Alisema baada ya kuona tatizo lilivyo kubwa la wanawake, ambao wanadhulumiwa mali za wenza wao baada ya kufariki, kamati iliyokuwa ikisikiliza wajane hao iliandika mapendekezo ya sheria ya mirathi na imekabidhiwa kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 

“Baada ya kamati niliyounda kusikiliza madai ya mirathi tulikuta tatizo ni kubwa, hivyo tuliandika taarifa tukamkabidhi Ummy Mwalimu pia tukaomba sheria ya mirathi itamke kuwa endapo baba atatangulia mbele ya haki basi mama awe ndio msimamizi wa mirathi,” amesema Makonda.

 

Alisema Sheria ya Ndoa ya Tanzania, imerithiwa kutoka India na ina zaidi ya miaka 120, hivyo sheria ikimpa haki mama lazima atampa mali mwanaye, si kama baba wadogo au shangazi wanavyokuwa wasimamizi wanavyofanya mali hizo kuwanufaisha wao na familia zao na kuwaacha walengwa wakitaabika.

 

Makonda pia aliwataka wanawake kuwa walezi wazuri wa watoto wao, hata kama wametekelezwa, kuliko kuwajaza maneno yenye uchungu waliokutana nao baada ya kutelekezwa, kwani kufanya hivyo kunasababisha kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili.

 

“Mama unamtolea mtoto wako maneno yenye uchungu baada ya kutelekezwa na baba yake, huyo mtoto haimuhusu kwani kila wakati mnakutana hakuwepo hivyo pambana na hali yako maana tunawafanya watoto waone maisha ndio yalivyo, wengine wanakataa kuolewa wakidhani wanaume wote wako hivyo,” alisema.

 

“Televisheni zimeleta malezi mengine kwa watoto wetu bila hata kwenda nje ya nchi wameiga tabia ambazo ni kinyume na maadili yetu hivyo wazazi jengeni tabia ya kuzungumza na watoto wenu na kufuatilia mwenendo wake, usingoje kujua tabia za mwanao kutoka kwa dada wa kazi au jirani,” aliongeza.

 

Alisema wanawake wanatakiwa kupambana na utamaduni wa makabila unaokataza wanawake kurithi mali, mfumo dume na kuishi kwa kusubiri kuambiwa unaweza bali mwanamke ajikubali kuwa anaweza bila kuambiwa na mtu.

 

Aliwataka wanawake kujiimarisha kiuchumi kwani akiwa na kipato hatonyanyasika, na kueleza kuwa katika kila halmashauri kuna mikopo isiyo na riba wanayoweza kukopa na kwa mwaka jana hadi sasa zaidi ya Sh bilioni 40 vimekopeshwa.

 

Kila mwaka Machi 8 ni Siku ya Wanawake Duniani na ilianza kutokana na jitihada za wanawake 15,000 mwaka 1908 walipoandamana jijini New York nchini Marekani, wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura.

 

Mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake jijini Copenhagen nchini Denmark walikubaliana kwa pamoja na mara ya kwanza ilisherekewa mwaka 1911, Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi. Sherehe ya 100 ilifanyika mwaka 2011, hivyo mwaka huu ni sherehe ya 107 ya wanawake duniani na kitaifa imefanyika mkoani Simiyu ambako mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Leave A Reply