The House of Favourite Newspapers

Makonda: Wasio na Kitambulisho cha NIDA, Namba ni Wambea

0

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  amesema wananchi wa mkoa huo ambao hadi jana Jumapili Januari 19, 2020,  hawana vitambulisho vya taifa wala namba waliendekeza zaidi umbea kuliko kufuatilia mambo ya msingi.

 

Amesema imekuwa tabia kwa Watanzania wengi kuhangaika na mambo yasiyo na msingi na kusahau vitu vya muhimu vinavyohusu usalama wao na taifa.

 

Makonda ametoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Zakhem-Mbagala katika tamasha la Maisha ni Kidole lililolenga kuhamasisha usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

 

Ili uweze kusajili laini ya simu kwa alama za vidole ni lazima uwe na kitambulisho cha taifa au namba. Leo Jumatatu, Januari 20, 2020 laini za simu ambazo hazijasailiwa kwa alama za vidole zitazimwa.

 

Makonda ametoa kauli hiyo baada ya kutaka wasio na namba za vitambulisho hivyo kunyoosha mikono, idadi kubwa ya wananchi kunyoosha ikiashiria kuwa hawana.

 

“Ninafahamu shughuli hii si mpya, wengi tunapenda kufanya mambo siku ya mwisho tena kwa kusubiri adhabu. Lazima tuwe werevu wa kuyajua mambo, bahati mbaya tumehamia kwenye umbea badala ya mambo yanayohusu maisha yetu.

 

“Unaposubiri hadi ushurutishwe au utishwe maana yake hujui manufaa ya teknolojia katika maisha yako. Kwa tabia hii ndio maana rais wetu anapata wakati mgumu kueleweka, tunatumia muda mwingi kufuatilia mambo yasiyotuhusu na si kulinda usalama wa taifa lako na maisha yako,” alisema Makonda.

 

Kuhusu matumaini ya kuongezwa muda Makonda amesema: “Kuna wanaosubiri kuongezwa siku sasa kwa taarifa yenu haiongezwi hata nukta, hatuwezi kuwa na tabia hii kama tunataka maendeleo. Yaani kusajili laini yako hadi tukuitie wanamuziki, hii ni aibu.  Haya mambo yanahusu usalama wako na taifa. Tatizo lenu mnataka maneno matamu,  sasa sina muda huo maana sitafuti kura kwako.”

 

Makonda amedai hadi leo watu milioni saba wana namba au vitambulisho lakini hawajajisajili.

 

“Watu wanajua nyumba za wageni bila kuelekezwa kuliko wanavyojua vitambulisho vya NIDA (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa).

 

Watu mnapenda umbea kuliko maisha yenu. Sijaja hapa kuwatia moyo nimekuja kuwashangaa, wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam tubadilike, waambieni na wenzenu kesho ndiyo mwisho.”

WAUMINI MLIMA WA MOTO WALIVYOPEWA ZAWADI WOTE , “NI BARAKA ZA BWANA”

Leave A Reply