Makundi 2 Kuamua Mshindi Uchaguzi 2020

DAR ES SALAAM: Wakati Tanzania ikielekea kufanya Uchaguzi Mkuu wa sita tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992, makundi makubwa mawili yametajwa kuwa na kura turufu (veto) katika chaguzi zote jambo ambalo wagombea udiwani, ubunge na urais wameaswa kuyazingatia.

 

RISASI linachambua.

Katika chaguzi zote makundi hayo ya vijana na wanawake, yametajwa kuongoza kwa kuwa na wapiga kura wengi ikilinganishwa na makundi mengine ambayo hushiriki kwa kusuasua katika chaguzi hizo.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mwaka 2015 inaonesha kuwa wapiga kura vijana waliokuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 35 walikuwa asilimia 57 ya wapiga kura wote.

 

Wapiga kura waliokuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 walikuwa asilimia 18 pekee, hao wengine asilimia 25 walikuwa na umri wa kati ya miaka 36 na 50. Takwimu hizo zilionyesha wapiga kura wanaume ni asilimia 47 na wanawake asilimia 53, ikiwa na maana kwamba wanawake ni wengi kushinda wanaume zoezi la upighaji kura.

 

VIJANA

Wakati kundi la vijana likionekana kuwa na kura turufu ya ushindi kwa wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais, baadhi ya wachambuzi waliozungumza na RISASI wamebainisha kuwa kundi hilo ndilo lenye uhitaji mkubwa zaidi ikilinganishwa na makundi mengine.

 

“Kundi hili la vijana linajumuisha vijana wanaofanya shughuli za bodaboda na umachinga. Lakini kundi hili ndilo lile lenye hasira ya kupigwa chini katika nafasi mbalimbali za ajira.

 

“Ndilo kundi lenye uhitaji mkubwa wa kujijenga kimaisha, kuanzia ujenzi wa nyumba na mahitaji mengine muhimu ambayo inaandaliwa misingi katika umri wa ujana.

 

“Kwa maana hiyo ni dhahiri kuwa kundi hilo ndilo linalotakiwa kutazamwa zaidi na wagombea hawa ili kuweza kuwashibisha hoja zitakazogusa maisha yao na kuhamasika kuwachagua,” alisema Francis John ambaye ni mmoja wa wachambuzi wa siasa.

 

WANAWAKE

Licha ya kwamba wanawake wanaingia pia katika kundi la vijana, ila kiujumla wanawake nao wamekuwa ndio kundi muhimu katika upigaji kura. Itakumbukwa kuwa kati ya wapiga kura milioni 23.2 waliojiandikisha mwaka 2015, asilimia 47 walikuwa wanaume na asilimia 53 walikuwa wanawake.

 

Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa, Omari Shulenga alisema kundi hilo limebeba matumaini ya vyama vya siasa kupata ushindi.

 

Wakati CCM ikionekana miaka mingi kuwa imewekeza kwa wanawake na wazee, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, mgombea urais wa upinzani Edward Lowassa alionesha ushindani mkubwa kwa kupata kura milioni sita ilihali mgombea wa CCM Dk. John Magufuli akipata kura milioni nane.

 

Hata hivyo, kundi la wanawake sasa limeendelea kuonekana kuwa muhimu kutokana na ushawishi wake ndani ya jamii.

 

“Tunaona wanawake ndio walezi wa familia, waangalizi wa kila kitu ndani ya jamii ikilinganishwa na wanaume. Ndio maana wanasiasa au wagombea wanatakiwa kutazama kundi hilo ambalo mbali na kuwa wamachinga, ndio mama lishe wa maeneo mengi nchini,” alisema.

 

Hoja hiyo iliungwa mkono pia Mhadhiri wa historia wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Tabora Francis Daudi, kwa kuongeza kuwa jambo la msingi kwa wagombea hao ni kuzungumzia mambo yanayogusa kwa undani makundi hayo mawili ili kuweza kuvuna kura za kutosha.

 

“Hakika huu ni uchaguzi wa vijana. Vyama vyote na wagombea wao wakiweza kuwashawishi vijana wana nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Kundi la wapigakura wapya zaidi ya milioni saba ni kubwa mno. Mbinu zitategemea matamanio ya kundi hili.

 

Hapa maana yake iwapo wamejiandikisha kupiga kura wengi wao walizaliwa miaka 1990. Kundi jingine la waliozaliwa mwanzoni mwa miaka 2000. Hayo ni mabadiliko, ni sura mpya ya wapigakura, kampeni zinagusa hao wenye uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.

 

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapigakura halali ni milioni 29.8 ikilinganishwa na milioni 23.1 kwa mwaka 2015.

Toa comment