MAKUNDI YA KOMEDI YANAYOFANYA POA BONGO!

COMEDY (komedi) ni neno la Kingereza lenye asili ya Ugiriki likimaanisha futuhi au ucheshi kwa Kiswahili.

Ni vichekesho vyenye lengo la kufurahisha, lakini pia kufundisha. Kuna wakati komedi zilijizolea umaarufu mkubwa Bongo na kufanya vijana wengi kuingia kwenye sanaa ya vichekesho.

 

Wachekeshaji wana umuhimu wa aina yake kwenye maisha. Ndiyo hutufanya tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni na mitandaoni au hata kukutana nao mitaani. Kwa kutuchekesha, nao hupata mkate wao wa kila siku na kuajiri kundi kubwa kwa vijana kwa sasa.

 

Miaka ya 1990, baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni, viliibuka vipindi vya ucheshi vya akina Mzee Small, King Majuto, Onyango na wengine ambao waliburudisha vilivyo. Baadaye waliibuka Mpoki na Joti kisha Max na Zembwela na Mizengwe yao.

 

Katika makundi ya komedi yaliyoibuka miaka ya 2000, ukiacha lile la Ze Comedy ambalo baadaye lilijulikana kama Orijino Komedi likiwa na watu kama Masanja Mkandamizaji, Joti, Mpoki, Wakuvwanga, Vengu na MacRegan ambalo sasa halipo, yapo makundi ambayo kwa muda mrefu yamekuwepo kwenye gemu na kufanya poa kama ifuatavyo;

1: MIZENGWE

Moja ya makundi bora na yaliyodumu kwa muda mrefu kwenye ucheshi ni Kundi la Kashkashi kupitia mchezo wao wa Mizengwe unaoruka kwenye Televisheni ya ITV.

Kundi hili linaundwa na vichwa vikali kama Sumaku, Mkwere Orijino, Mzee Matata, Maringo Saba na mwanadada pekee, Safina. Mchezo wao huo ambao hutofautiana topiki kila wiki hupendwa na watu wa rika zote kuanzia watoto hadi watu wazima. Hawa jamaa hawachekeshi tu, bali pia hutoa mafunzo kwenye jamii. Katika kundi hilo, Sumaku anatajwa kuwa ndiye injini.

 

Kabla ya kubakiwa na wakali hao, walikuwepo wengine kama Max aliyetangulia mbele ya haki, Zembwela, Bi Kiroboto na Masele Chapombe waliojichanganya kwenye maisha mengine.

Mmoja wa waanzilishi wa kundi hili, Zembwela ambaye ni mtangazaji wa Televisheni ya EATV na East Africa Radio anasema makundi yote yanaweza kuvunjika, lakini Mizengwe litadumu kwa sababu kwenye vichwa vya waanzilishi hakukuwa na tishu bali kulikuwa na akili.

2: ZE COMEDY SHOW

Kundi hili lilipata nafasi kwenye Televisheni ya EATV baada ya kuvunjika kwa lile Kundi la Ze Comedy lililokuwa likiundwa na akina Masanja Mkandamizaji walioondoka na kwenda kuanzisha Kundi la Orijino Komedi lililokuwa likiruka kupitia TBC1 kabla ya kupotea kwenye ramani.

Kundi la Ze Comedy Show linaundwa na vichwa matata vya kuchekesha kama Mtanga, Bambo, Kiwewe, Shaban na Master Face.

 

Kama lilivyo Kundi la Mizengwe, Ze Comedy Show nao huruka mara moja kwa wiki ambapo mbali na kuburudisha pia hutoa elimu kuhusu mambo mbalimbali ya kijamiii.

Mmoja wa memba wa kundi hilo, Mtanga aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, kuna kazi rahisi, lakini siyo kuvunjika kwa Ze Comedy Show kwani lina misingi imara na hubebwa na nidhamu ya kazi.

3: VITUKO SHOW

Kule kwenye Televisheni ya Channel Ten kuna jamaa wanaounda Kundi la Vituko Show. Kundi hili kwa muda mrefu lilibebwa na vituko vya uswazi vya kubandika na kubandua likiwa chini ya Kampuni ya Al-Riyam. Ndilo kundi lililoundwa na wasanii wengi zaidi ukilinganisha na makundi mengine ya komedi.

 

Vituko Show ambalo kwa sasa limesimama kidogo, kwa miaka mingi limedumu kwenye gemu huku likikumbwa na misiba mingi kwa kupoteza ‘mashine’ zake zilizotangulia mbele ya haki kama Sharo Milionea, Kinyambe, King Majuto, Mjomba Kundambanda na kubakiwa na wasanii kama Masele Chapombe, Asha Boko, Man Dizo, Thabitha, Eric Kisauti, Kazi na wengineo.

Kama yalivyo makundi mengine, Vituko Show nalo hufanya kazi ya kuburudisha na kuelimisha mambo mbalimbali hasa yale yanayojiri uswahilini.

4: FUTUHI

Unapozungumzia makundi ya kuchekesha Bongo, kule jijini Mwanza lipo moja matata mno linaloitwa Futuhi.

Kama yalivyo makundi mengine, Futuhi nalo hurusha kipindi chake mara moja kwa wiki kupitia Televisheni ya Star TV.

Ukiondoa waliotangulia mbele ya haki wawili, Mzee Dude na Kalume Kenge, kundi hilo kwa sasa linaundwa na wasanii wakali kama Brother K, Sharobaro wa Kihaya, Mama Njelekela, Gongalai, Mjaluo na Njelekela ‘Emoro’.

5: TIMAMU

Memba wanaofanya vizuri kwa sasa kwenye komedi mtandaoni ni wale wanaounda Kundi la Timamu. Kwa sasa kundi hilo limebakiwa na memba wawili, Mjeshi na Mr Beneficial baada ya Ebitoke na Mkali Wenu kusepa na kwenda kutafuta maisha kwingine.

Timamu wao hawaruki kwenye kisimbusi kama makundi mengine bali wanaonekana kupitia mtandaoni na shoo mbalimbali za majukwaani, lakini bado wanakamata kinoma.

‘KONKI MASTER’ ya Dudu Baya Yatikisa Morogoro!


Toa comment