The House of Favourite Newspapers

Mali: Jeshi Laigomea ECOWAS Kumrudisha Rais Keita

0

MAZUNGUMZO nchini Mali yanayolenga kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea kufuatia mapinduzi yaliofanyika wiki iliopita yamemalizika bila makubaliano huku viongozi wa Jumuia ya Kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) wamesema kwamba rais aliyeondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita, arudishwe madarakani.

 

Lakini wajumbe hao wa Ecowas walishindwa kuwaelewesha viongozi hao wa jeshi kwamba huo ndiyo uliokuwa uamuzi mzuri. Keita alikabiliwa na maandamano makubwa kabla ya mapinduzi yake na raia wengi nchini Mali wameunga mkono kuondolewa kwake.

 

Msemaji wa Jeshi Kanali Ismael Wague alinukuliwa na Reuters akisema kwamba baada ya mazungumzo kwisha uamuzi wa mwisho kuhusu serikali ya mpito utatolewa na raia wa Mali wenyewe.

Lakini wazo la Keita kurudi madarakani huenda lilikataliwa na yeye mwenyewe, kulingana na chombo cha habari cha AFP.

Taarifa tofauti kutoka kwa pande hizo mbili zilisema kwamba rais huyo amekuwa katika kizuizi tangu mapinduzi hayo Jumanne iliopita na kwamba hangetaka kurudi madarakani.

Kundi la wapatanishi linaloongozwa na aliyekuwa rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, litaripoti kwa viongozi wa serikali za Afrika kuhusu hatua zilizopigwa kulingana na Kanali Wague.

 

Mazungumzo hayo yalianza kwa maelezo machache siku ya Jumamosi na kuendelea siku ya Jumapili na Jumatatu. Mwisho wa kikao Bw.  Jonathan alisema: Tumeafikiana baadhi ya makubaliano lakini hatujapata mwafaka kuhusu masuala yote.

 

Wiki iliopita, maelfu ya raia waliandamana katika barabara za mji mkuu wa Bamako ili kusherehekea mapinduzi hayo ambayo yalishutumiwa kote duniani. Keita alishinda muhula wa pili katika uchaguzi wa 2018, lakini tangu mwezi Juni amekabiliwa na maandamano makubwa kuhusu ufisadi , usimamizi mbaya wa uchumi na mizozo ya uchaguzi wa bunge.

 

Kumekuwa na hasira miongoni mwa wanajeshi kuhusu mishahara yao na vita dhidi ya Wanajihad katika eneo la kaskazini la taifa hilo ambapo mamia ya wanajeshi wameuawa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Leave A Reply