The House of Favourite Newspapers

Malinzi: Tumekosea kuiruhusu Azam

0

Rais-wa-Shirikisho-la-Mpira-wa-Miguu-Jamal-Malinzi-akioneshwa-kukerwa-na-waamuzi-kuuza-mechi-600x360Said Ally, Dar es Salaam
KUFUATIA malalamiko ya klabu kadhaa za Ligi Kuu Bara juu ya Azam FC kuruhusiwa kwenda nchini Zambia wakati ligi hiyo ikiendelea, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeibuka na kuomba radhi juu ya kitendo hicho.

TFF iliipa ruhusa Azam kwenda Zambia kushiriki michuano maalumu iliyoandaliwa na timu ya Zesco ya nchini humo ambapo kikosi hicho kiliondoka Jumatatu ya wiki hii na kusababisha michezo yao miwili kupigwa kalenda, hali ambayo imezua taharuki miongoni mwa timu za ligi kuu ambazo nazo zimekuja juu na kutaka zipewe ruhusa ya kusafiri.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi, jana alizungumza na wanahabari na kusema kuwa wanaziomba radhi timu za ligi kuu kwa kitendo kilichotokea cha kuipa ruhusa Azam kwa kuwa hakikuwa katika utaratibu mzuri.

“Kiukweli tunaomba radhi kwa kitendo ambacho tumekifanya kwa kuipa Azam ruhusa ya kwenda Zambia hali ambayo imezua taharuki kwa timu nyingine na kusababisha wao pia kuomba ruksa ya kwenda nchi mbalimbali, lakini tutajitahidi kuwabana pale watakaporudi kwa kuwachezesha mara mbili kwa wiki ili kuwafanya wawe sawa kimichezo na wenzao.

“Lakini niseme tu kuwa tumekosea kwa Azam lakini hatutaki kuona timu nyingine zinachukulia mwanya huo nao kuleta barua zao kwa kutaka kwenda nje ya nchi kama ilivyofanyika kwa timu hiyo.

“Hatutakuwa tayari kufanya jambo ambalo tumelikosea na tunasema hatutaipa ruhusa timu yoyote ile hata hawa Yanga ambao nimesikia wanaomba kwenda Afrika Kusini safari hiyo haitakuwepo, watambue hilo,” alisema Malinzi.

Leave A Reply